Wakulima wa pamba iliyoimarishwa walia kukawia kwa mbegu

Wakulima wa pamba iliyoimarishwa walia kukawia kwa mbegu

NA SAMMY WAWERU

WAKULIMA wa pamba nchini wamelalamikia kucheleweshwa kuwasili kwa mbegu ili kuanza shughuli ya upanzi.

Msimu wa upanzi huanza mwezi Oktoba, wakulima wengi wakitegemea mvua.

Aina ya mbegu zinazokuzwa nchini ni zile asilia na zilizoboreshwa (BT Cotton).

Miaka miwili iliyopita, serikali iliidhinisha na kuruhusu kulimwa nchini kwa pamba iliyoboreshwa kupitia tafiti na mfumo wa msimbo jeni.

Jumatatu, Rais William Ruto aliondoa marufuku ya miaka 10 iliyozuia uagizaji wa bidhaa za kula za GMO.

Mwaka huu hata hivyo wakulima wa pamba wanateta kucheleweshewa mbegu.

“Mwaka huu hatujapokea mbegu za pamba wakati ufaao, msimu wa upanzi ukibisha hodi,” akalalamika Munene Kamau, mkulima wa pamba eneo la South Ngariama, Kirinyaga.

Kamau hulima zao hilo linalotumika kuunda nguo na bidhaa zinginezo kwenye ekari tatu.

Munene Kamau, mkulima wa pamba eneo la South Ngariama, Kirinyaga. PICHA | SAMMY WAWERU

Mkulima huyo alitoa lalama hizo wakati wa mkutano na wadauhusika katika sekta ya mazao yaliboreshwa kupitia mifumo na teknolojia za kisasa.

“Wengi wetu tunaotegemea msimu wa mvua, tukikosa kupokea mbegu mwezi huu ina maana kuwa tutasubiri hadi 2023,” akasema Margaret Nyaga kutoka Embu.

Mbegu za pamba iliyoboreshwa huagizwa kutoka India.

“Tunajaribu tuwezavyo kuona zinaingia nchini muda ufaao na kusambazwa,” akaahidi Japhet Nteere, afisa wa kilimo kutoka serikali ya kitaifa.

Serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt Ruto imeahidi kufufua kilimo cha pamba nchini.

Sekta hiyo ilikuwa maarufu na tajika wakati wa Rais mstaafu hayati, Mzee Daniel Arap Moi.

  • Tags

You can share this post!

Rais aanza kutekeleza ripoti ya BBI taratibu

Napoli yatoka nyuma na kudhalilisha Ajax mbele ya mashabiki...

T L