Habari Mseto

Wakulima wahimizwa kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa za mifugo

September 20th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

WAKULIMA wametakiwa kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa za mifugo iwapo wanataka kuimarisha shughuli za ufugaji hasa mifugo kwa ajili ya uzalishaji nyama na maziwa.

Akizungumza Jumatano wakati wa uzinduzi wa kiwanda kipya cha kutengeneza madini ya mifugo cha Cooper K – Brands Ltd, CKL, mkurugenzi mkuu Mucai Kunyiha alisema kuwepo kwa bidhaa bandia sokoni ni miongoni mwa visababishi vikuu vya mazao duni.

Alisema changamoto hiyo itaangaziwa iwapo wakulima watakuwa makini wanaponunua madini na kushirikiana na asasi husika katika vita dhidi ya bidhaa bandia.

“Ninawashauri wawe waangalifu kwa sababu soko limesheheni bidhaa bandia hasa madini ya kuimarisha afya ya mifugo. La sivyo wataendelea kulalamikia mazao duni na ya hadhi ya chini,” akasema Bw Kunyiha wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho eneo la Tatu City, Ruiru kaunti ya Kiambu.

Kunyiha hata hivyo alipongeza serikali katika jitihada zake katika vita dhidi ya bidhaa bandia nchini, akisema sekta ya kilimo na ufugaji ni baadhi ya zilizoathirika pakubwa.

Baadhi ya wakulima wamekadiria hasara mifugo wao kufariki na kupata mazao duni kwa sababu ya madini bandia na ambayo hayajaafikia vigezo vifaavyo.

Sura mpya

Ili kukabiliana na suala hilo – hasa kuzuia matapeli kuuza madini bandia kwa jina la kampuni hiyo – CKL pia ilizindua upakiaji na sura mpya ya bidhaa zake.

Kupitia sura mpya, Bw Kunyiha alisema hatua hiyo itasaidia wafugaji kutambua bidhaa zao upesi.

CKL ni tajika nchini katika utengenezaji wa madini hasa chumvi ya kuimarisha mifugo wa maziwa na nyama kama Maclik Super, Maclik beef, Maclik dry cow, Maclik XP na Maclik mineral brick. Pia hutengeneza na kusambaza dawa kama triatix, grenade, nilzan, kupakula, nefluk, romectin na nyinginezo.

Kiwanda kilichozinduliwa kimegharimu kima cha Sh700 milioni, ikiwemo mitambo na mashine za teknolojia ya kisasa kuunda madini. CKL ilishirikiana na Africa Agriculture and Trade Investment Fund (AATIF) na KFW Development Bank kufanikisha ufadhili wa shughuli hiyo.

Aidha, kinapaniwa kubuni nafasi 20 za ajira ya moja kwa moja na zaidi ya 800,000 kwa wakulima watakaofaidika nacho.