Habari Mseto

Wakulima waililia kaunti iwachimbie mabwawa

September 6th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

WAKULIMA katika kaunti ya Mombasa wameiomba serikali iwachimbie mabwawa ili waweze kuendeleza kilimo hata wakati wa kiangazi.

Wakizungumza na Taifa Leo, wakulima hao kutoka eneo la Kashani, kata ndogo ya Bamburi walisema kuwa tatizo lao kuu ni ukosefu wa maji.

Mkulima mmoja, Khamis Chembe,43, alisema kuwa kilimo cha mboga za kienyeji kama vile mchicha na mnavu kimepungua kwa kuwa wakulima hawana maji.

Alisema kuwa mifugo nao wanahangaika kwa kukosa maji safi, na chakula cha kutosha msimu huo wa kiangazi.

“Baadhi ya wakulima wamejitolea na kuchimba visima vyao wenyewe. Hata hivyo, baadhi ya visima hutoa maji ya chumvi ambayo hayakuzi mimea. Tukichimbiwa mabwawa, yataweza kuzuia maji ya mvua tutakayoyatumia kunyunyizia mimea yetu hata msimu wa kiangazi,” akasema Bw Chembe.

Wakulima katika eneo hilo wanapanda mboga kwa wingi na kufuga wanyama kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Hata hivyo, Bw Chembe aliilaumu wizara ya kilimo katika kaunti kwa kuwatenga katika baadhi ya miradi kama vile utoaji wa mbegu, mbolea, dawa za kunyunyizia mimea na mifugo.

Alisema wakulima wa pale wamekosa mafunzo ya jinsi ya kuimarisha kilimo.

“Kamati za kilimo hazijawahi kufika huku kwetu kujua ni shida zipi tunapitia kama wakulima. Tumetengwa sana na viongozi wetu haswa walio katika sekta ya kilimo. Tunawaomba watutembelee ili wajue mambo tunayohitaji kuboresha ukulima katika kaunti hii,” akasema Bw Chembe.

Mwenzake, Bw Enos Msungu ambaye amejitosa katika kilimo cha mboga na matunda alisema kuwa wanaweza kulima chakula cha kuwatosha wakazi wa kata hiyo iwapo watapata usaidizi wa kutosha kutoka kwa kaunti.

Bw Msungu alisema kuwa watatengeneza vikundi vya wakulima wa eneo hilo ili ajenda wanazozungumzia ziweze kuwasilishwa rasmi kwa wizara ya kilimo.

“Tukiungana pamoja itakuwa rahisi kuwavutia viongozi wetu, waje wajionee kazi zetu, na waangalie ni jinsi gani watatusaidia tuimarishe kilimo. Tumejitolea katika ukulima na maono yetu ni kuweza kupanda chakula kitakachoweza kutosheleza wakazi wote wa kaunti ya Mombasa,” akasema.