Habari Mseto

Wakulima wakataa sheria mpya za kilimo cha kahawa

September 8th, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

VIONGOZI wa mashirika ya kahawa katika kaunti ya Kirinyaga jana walikataa sheria mpya za kahawa za mwaka wa 2019, zinazolenga kurekebisha hali mbaya ya kilimo cha kahawa nchini.

Kanuni hizo tayari zimenukuliwa na serikali kuu.

Wenyekiti 15 wa mashirika ya kahawa walilalamika kwamba kikosi maalum kilichoundwa na Rais Uhuru Kenyatta kuangalia maswala yanayokumba kilimo cha kahawa, hakikuwahusisha wala kupata maoni yao.

Viongozi hao walitishia kwenda kortini kuzuia utekelezaji wa kanuni hizo ambazo walidai zitakuwa mbaya kuliko zile za zamani.

Walisema malipo ya mfumo wa moja kwa moja kwa wakulima kama moja ya kanuni mbaya zaidi.

Katika mfumo huu, pesa zingewekwa katika akaunti ya shirika kubwa la kahawa na baadaye kila mkulima kutumiwa haki yake baada ya ada kutozwa.

Viongozi hao walisema hakukuwa na mwongozo wa wazi kuonyesha ni nani atakayeendesha mfumo huo.

“Mfumo huu sio mzuri kabisa. Tulipaswa kushauriwa kabla ya kanuni hizo kujumuishwa,” mwenyekiti wa shirika la kahawa la Rung’eto, Bw Fredrick Waweru alisema.