Wakulima wakosa soko kwa zao lenye madini muhimu kwa afya ya binadamu

Wakulima wakosa soko kwa zao lenye madini muhimu kwa afya ya binadamu

Na SAMMY WAWERU

MIAKA mitatu iliyopita, Moses Gitonga alikuwa na matumaini tele alipoanza kilimo cha maboga asilia kwa sababu utafiti aliofanya ulifanya aamini maboga maarufu kama malenge ni kati ya mimea rahisi kupanda, kutokana na gharama yake ya chini.

Alijawa matumaini kwamba maboga hayo “yana mapato ya kuridhisha”.

Ni mmea wa kienyeji usiohitaji kemikali vile kwa sababu ya ustahimilivu wake dhidi ya magonjwa na wadudu.

Anafichua, safari ya kukuza maboga ilianza 2019, Gitonga akidokeza kwamba alipania mazao yake yawe kati ya lishe ya familia yake.

“Nilipewa mbegu na kaka yangu, nikapanda punje 40 kwenye thumni ekari, (1/8). Mazao niliyopata yaliridhisha,” Gitonga asema.

Anaeleza kwamba gharama haikuzidi Sh1,500, inayojumuisha mbolea na leba, akifichua alivuna karibu kilo 1, 000.

“Yalinishawishi kugeuza maboga kuwa kilimo-biashara,” anasema mkulima huyo ambaye amewahi kuhudumu kama afisa wa kikosi cha jeshi nchini, KDF.

Katika kijiji cha Nagum, Kaunti Ndogo ya Gilgil, Kaunti ya Nakuru Gitonga anamiliki ekari tatu, na anasema nusu yake ametengea kilimo cha maboga.

Mkulima Moses Gitonga (kulia) na ambaye hukuza maboga akiwa na mfanyakazi wake shambani mwake Nagum, Gilgil. PICHA | SAMMY WAWERU

Kwenye ekari moja na nusu, anatarajia kuvuna zaidi ya tani 15, sawa na kilo 15, 000.

“Niligawanya shamba ili nivune vipindi tofauti,” Gitonga anasema, akidokeza kuwa ana tani zingine 5 zaidi kwenye ghala.

Furaha aliyokuwa nayo awali alipoingilia kilimo cha maboga inaendelea kufifia, kutokana na ukosefu wa soko la mazao.

Licha ya kuwa ni zao lenye tija tele kiafya, mahangaiko anayopitia kutafuta soko yameishia kutambua “malenge ni mimea yatima”.

“Mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenyatta ni kuangazia usalama wa chakula nchini. Kati ya mimea inayotajwa kupigwa jeki, maboga hayapo. Ni yatima, yamepuuzwa. Serikali imeegemea kwa kahawa, majanichai, miraa na maua,” Gitonga analalamika.

Anasema changamoto za soko anazopitia, uchunguzi aliofanya unaashiria zinakumba wakulima wengine.

“Maboga ni mimea muhimu, ambayo mikakati kabambe ikiwekwa kuangazia kero ya soko ukuzaji wake utakuwa kilimo-biashara. Yanaweza kuhifadhiwa kipindi cha muda wa mwaka mmoja baada ya mavuno, hayahitaji kuwekwa dawa zenye kemikali ili kudumu kama vile nafaka hufanywa ili kuhifadhika. Changamoto za soko zinazonikumba, ni sawa na za mamia ya wakulima wengine nchini,” anaelezea mkulima huyo ambaye pia ni mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu.

Kulingana na Gitonga, kufikia sasa ameweza kuuza tani 5 pekee.

“Yalinunuliwa na shule kadha Gilgil,” anadokeza.

Anasema wanunuzi anaopata wanaagiza maboga ya saizi ndogo, ili kuyakata na kuuza vipande vidogo.

Wanaepuka yale makubwa kwa sababu yatachukua muda mrefu kuisha, na pindi yanapokatwa huoza upesi.

“Maboga yangu yana uzani wa kati ya kilo 5 – 30. Mbali na wateja rejareja, nimejaribu wa kijumla, mahangaiko ni yale yale,” asisitiza.

Huku bei yake ya lango la shamba ikiwa kati ya Sh70 – 100 kwa kilo, Gitonga anapata oda za Sh6 – 10 kwa kilo.

Anakadiria gharama kuzalisha kilo moja ya boga ni Sh28, hivyo basi ofa anayopata itampeleka hasara.

Amekumbatia mfumo wa kilimohai kuyakuza.

“Tangu niingilie kilimo cha maboga, sijashuhudia magonjwa. Wadudu huwadhiti kwa kutumia mbinu asilia,” anafafanua.

Hutumia maji ya mto ulio karibu na shamba lake, ila nyakati za ukame hukauka. “Nina zaidi ya chupa 5, 000 za plastiki, zilizotumika, ambapo huziweka maji zinayadondoa kidogo kidogo (drip-bottles) kwenye mashina ya miboga,” aelezea.

Maboga hukomaa kati ya miezi mitano hadi sita baada ya upanzi.

Wakulima wanahimizwa kutumia mbegu za maboga yaliyokomaa kwa minajili ya upanzi. “Yawe na afya bora. Mbegu zikaushwe kabla ya kuzipanda,” anashauri Daniel Wanjama, mratibu katika muungano wa kitaifa wa wazalishaji mbegu.

Kulingana na Wanjama, hakuna mbegu maalum zilizoidhinishwa za maboga.

Huku kero ya soko ikiwa kikwazo kikuu kwa mkulima Gitonga, anasema amebaini suluhu ni kuyaongeza thamani.

“Kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, ninaendeleza utafiti wa kuongeza maboga thamani,” anadokeza.

Anaendelea kueleza: “Sijaweza kukumbatia mfumo huo kwa sababu unahitaji mtaji mkubwa. Maboga yanaweza kukaushwa, kusagwa na kuchanganywa na unga wa nafaka aina nyingine kama vile mahindi na ngano, ili kuongeza virutubisho. Ni hatua inayohitaji mashine na ambazo ni ghali.”

Kwa mujibu wa masimulizi yake, hatua hiyo ina maana kuwa anahitaji mashine maalum ya kukausha (dehydrator), ya kusaga na kuchanganya kitaratibu na unga mwingine.

Vile vile, anahitaji ya kupakia.

“Isitoshe, mbegu na majani ya maboga nitaweza kuyakausha na kuyasaga kuwa unga,” anasema.

Ni mikakati anayosema akiweza kuafikia, kitakuwa kiwanda kikubwa na kitakachowafaa wakulima wenza nchini.

“Ninachohitaji kwa sasa ni mwekezaji mwenye mawazo na maono kama yangu, tushirikiane kuanzisha mpango huo na ambao utaokoa wakulima wa maboga nchini,” asema.

You can share this post!

MKU kushirikiana na shule spesheli ya St Patrick’s...

Shujaa yarejea nyumbani na majeraha

T L