Habari Mseto

Wakulima walia kuhangaishwa kupata mbegu na mbolea

April 1st, 2019 2 min read

RICHARD MAOSI NA KEVIN ROTICH

WAKULIMA kutoka Kaunti za Nakuru na Kericho wameomba serikali iwapunguzie gharama ya mbolea na mbegu wanapojiandaa kwa ajili ya upanzi msimu huu. 

Baadhi yao wanalalamikia bei ghali ya mbolea, dawa za kupulizia wadudu na miche. Tangu mvua ya rasharasha ianze katikati ya Machi maeneo ya Nakuru, wengi wao walianza kujishughulisha kwa kuondoa magugu shambani.

Taifa Leo Dijitali ilipozuru mashamba kadhaa viungani mwa mji wa Nakuru ili kubaini hali halisi, ilipata matrakta yakiwa kwa harakati za kulainisha mchanga huku wakulima wakisubiri mvua.

Wengi wao wanasema kila mara wanapotembelea Bodi ya Kitaifa ya Nafaka Na Mazao (NCPB), huelekezwa katika afisi za chifu wajiandikishe kwanza kabla ya kupata mbolea ya bei nafuu.

Wamekuwa wakihangaishwa wanapoenda kununua mbolea na mbegu.  James Chesang mkulima kutoka eneo la Kabarnet Farm Kabarak, Nakuru anasema alipoteza matumaini ya kutafuta mbolea zinazotolewa na serikali.

Wakulima kutoka eneo la Londiani, Kaunti ya Kericho wakiandaa mashamba yao wakitumia trakta. Picha/ Richard Maosi

“Siwezi kupata msaada wa mbolea ya serikali kwa sababu kila mara huwa ninaelezwa nijiandikishe na afisi ya chifu wa hapa,” alisema.

Anasema hana hakika iwapo atapanda msimu huu, kwani shamba lake ni kubwa na atahitaji mbolea nyingi pamoja na mbegu ambazo kumudu gharama si rahisi.

Pia alieleza kuwa kupata soko la bidhaa kama mahindi ni changamoto kubwa inayowakabili wakulima siku hizi .

Bei ya mahindi imekuwa ikibadilika kila wakati na kuwalazimu wakulima waanze kupanda vitu tofauti kwenye bonde la ufa kama vile ngano na nyasi .

Anaomba serikali ya kitaifa iwawezeshe wakulima wadogo kutoka mashinani wapate kujiinua kutokana na ukulima.

Trakta lakarabatiwa baada ya hitilafu kutokana na matayarisho ya mashamba msimu wa kupanda ukikaribia katika eneo la Kabarak, Kaunti ya Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Tulizungumza na mkulima mwingine kutoka eneo la Lanet, James Mugo ambaye alitoa malalamishi ya kujiandikisha na chifu.

“Sekta ya ukulima inaendelea kuzorota kwani washikadau wamegeukia njia nyinginezo za kujiajiri,” alisema.

Mzee Patrick Kabati kutoka kutoka eneo la Njoro anaomba serikali ijaribu kuelewa changamoto zinazowakabili wakulima.

Hili linajiri huku kiangazi kikizidi kuchelewesha msimu wa kupanda na kuwaletea hasara wakulima wengi.

Mimea imekauka na mifugo wengi kufa katika kaunti za Baringo na Samburu, licha ya serikali kuhakikishia wakazi kuwa inadhibiti hali.