Habari za Kitaifa

Wakulima walilia Gen Z iwatetee

Na TITUS OMINDE June 25th, 2024 2 min read

WAKULIMA wa ngano kutoka North Rift wamewataka vijana chipukizi na machachari wanoshiriki maandamno maeneo tofauti nchini, kuuliza serikali sababu za bei ya mkate kuendelea kupanda licha ya kiwango cha mazao kuongezeka mara dufu.

Wakionekana kuzongwa na maswali chungu nzima, wanashangaa ni kwa ni mfumko wa bei ya bidhaa hiyo muhimu unazidi kushuhudiwa ilhali mapato yao yangali chini.

Wakizungumza mjini Eldoret, wakulima hao walisema kinachowashangaza zaidi ni kuona bei ya vyakula vingine ikishuka huku mkate ukipanda.

“Wakati nchi yetu ilikuwa na changamoto ya mfumko wa bei ya bidhaa muhimu, mkate ulikuwa miongoni mwa bidhaa hiyo. Kinachoshangaza ni kwamba bei ya bidhaa zilizoathirika imeshuka ila ya mkate ingali juu,” akasema Bw Hassan Kipkosgei ambaye pia ni mfanyibiashara mjini Eldoret.

Kwa niaba ya wakulima wenza, Mzee Kipkosgei alihimiza vijana wa kizazi cha sasa maarufu kama Gen Z wanaoandamana kuwasilisha malalamishi yao kwa serikali.                                                                                                       Bw Kosgei almaarufu Assis, alisema juhudi za wakulima na wafanyibiashara kutaka kujua ni kwa nini bei ya mkate imepanda zaidi, zimekuwa zikiambulia patupu na ndio maana wameamua kutuma vijana kupata majibu.

Mkulima huyo alisema huenda serikali ikaskiza vijana na kutoa mwelekeo kuhusu bei ya mkate na bidhaa zingine za ngano.

Kauli yake ilijiri siku moja baada ya Rais William Ruto kuonekana kulegeza kamba kufuatia mgomo unaoendelea maeneo tofauti nchini kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024/2025 unaopendekeza nyongeza ya ushuru na ada kwa bidhaa muhimu za kimsingi.

Rais Ruto aliahidi kwamba atafanya kikao na vijana wa Kenya, ili kuangazia masuala yanayowakera.

Wabunge wataupigia kura kuupitisha au kuuangusha leo, Jumanne, Juni 25, 2024, na ukifua dafu utachochea maisha kuwa magumu.

Mzee Kipkosgei anapendekeza bei ya mkate kushukishwa hadi kati ya Sh40 na Sh50 kipimo cha gramu 400.

Alisema amekuwa akiuza ngano gunia la kilo 90 Sh1900, chini kutoka Sh2, 300 ambapo licha ya mabadiliko hayo bei ya mkate unazidi kupanda.

“Kwa nini mkulima ananunuliwa ngano bei ya chini ilhali akienda sokoni, mkate unakuwa ghali?” alishangaa Mzee Kosgei.

Maoni sawa na hayo yalitolewa na mkulima Tom Murgor kutoka eneo la Moiben, Uasin Gishu ambalo ni maarufu kwa kilimo cha ngano.

Bw Murgor alisema kwa miaka mingi bei ya mkate imekuwa ikikosa kuambatana na ya mauzo ya ngano.

Kulingana na Murgor, Gen Z itasaidia wakulima na watumiaji bidhaa za ngano kupata afueni ya bei kupunguzwa.

“Tumeona Rais akianza kuonyesha dalili ya kusikiza watoto wetu na tunatumai wao ndio wataokoa mkulima,” alisema.

Bw Murgor alisifia juhudi za vijana, akiwataja kama uzao wenye maono kwa taifa.

Alijiunga na Wakenya wengine kutahadharisha polisi dhidi ya kuwadhulumu wanapotetea haki yao Kikatiba.

Akikashifu polisi, alisema ni aibu kuona wanapiga ‘watoto’ ambao pia wanatetea haki zao.