Wakulima walilia serikali gharama ikizidi kupanda

Wakulima walilia serikali gharama ikizidi kupanda

NA BARNABAS BII

WAKULIMA wa nafaka watalazimika kukabiliana na gharama ya juu huku bei za mafuta, chakula na usafiri zikiongezeka kupindukia licha ya mageuzi yanayotekelezwa na serikali.

Mageuzi hayo yanajumuisha kutenga kiasi cha Sh3.55 bilioni ili kupunguza bei ya mifuko 1.4 milioni ya mbolea hadi Sh3,500 kutoka Sh6,500 kwa lengo la kubadilisha sekta hiyo kuwa uwekezaji wenye faida.

Wakulima wametaja hatua ya kuongezwa kwa bei za dizeli kama pigo kuu wakisema inaongeza gharama ya kuandaa ardhi, usafirishaji wa mavuno na kilimo kwa jumla.

“Kilimo cha mimea kama vile mahindi na ngano shughuli inayotumia mashine ambapo hatua ya kuongeza bei za mafuta itapandisha bei ya vifaa vya shambani kwa jumla,” alisema Bw Jackson Kiptoo, kutoka Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Wakulima wengi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, linalozalisha chakula kwa wingi nchini, wanakabiliwa na changamoto za kifedha wanapojiandaa kuvuna mazao ya mahindi na ngano msimu huu.

“Dizeli ndiyo kawi ya uzalishaji wetu wa mazao na kuongeza bei za dizeli na petroli kwa Sh20 kwa lita moja ni gharama ya ziada kwa wakulima ambao wanalazimika kugharamikia mambo mengine kama vile ukarabati wa mashine hivyo kufanya kilimo kukosa faida,” alisema Miriam Too, kutoka Cherang’any, Kaunti ya Trans-Nzoia.

Mamlaka inayosimamia Kawi na Petroli (EPRA) imepandisha bei hizo baada ya serikali ya Rais William Ruto kudokeza kuhusu mipango ya kuondoa ufadhili wa mafuta na kuashiria siku ngumu zijazo kwa Wakenya.

EPRA imebadilisha bei za mafuta huku lita moja ya petoli mjini Eldoret ikiuzwa kwa Sh179.5 kutoka 156.13 nayo dizeli ikiuzwa kwa Sh165.7 kutoka Sh147.32 na kuwapandishia gharama ya uzalishaji wanakandarasi wengi.

Inamgharimu mkulima Sh4,500 kulima ekari moja ya ardhi huku uzalishaji wa mfuko wa kilogramu 90 wa mahindi ukikadiriwa kuwa Sh1,700 kiasi ambacho ni cha juu zaidi katika eneo la Afrika Mashariki.

“Mahindi yamesalia kuwa chakula chetu cha kitamaduni na kitega uchumi ambapo itakuwa vigumu kustawisha uzalishaji kutokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta,” alisema Bi Alice Chesang, kutoka Chepkumia, Kaunti ya Nandi.

Wamiliki wa magari watakuwa wamelipa kiasi cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa cha Sh214.03 kwa kila lita ya petroli na Sh206.17 kwa dizeli pasipo ufadhili huo wa mafuta.

Mfuko wa kilogramu 10 wa mbegu za mahindi unauzwa kwa Sh2,000, kutoka Sh1,500 bei ya msimu uliopita wa upanzi huku mfuko wa kilogramu 25 ukiuzwa kwa Sh5,000 kutoka Sh4,750 na kuwazidishia wakulima wengi mashaka ya kifedha.

Mazao ya mahindi katika Bonde la Ufa yalishuka kutoka mifuko 21 milioni hadi mifuko 16 milioni msimu uliopita ingawa mazao mengine mbadala yaliongezeka.

  • Tags

You can share this post!

Ufaransa waponea kushushwa ngazi kwenye Uefa Nations League...

Ruto atangaza Baraza la Mawaziri, walioteuliwa sharti...

T L