Habari Mseto

Wakulima waliohodhi mahindi walia bei ikiendelea kushuka

May 31st, 2024 1 min read

Na BARNABAS BII

WAKULIMA wa nafaka katika eneo la North Rift ambao wamekuwa wakihifadhi mahindi ya thamani ya mamilioni sasa wamepata hasara huku bei ya bidhaa hiyo ikiendelea kushuka.

Wakulima hao ambao walihifadhi bidhaa hiyo kwa miezi kadhaa wakitarajia bei ipande sasa wanataka Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kuwalipa Sh4,000 kwa kila gunia la kilo 90.

Gunia la mahindi la kilo 90 lilikuwa likiuzwa kwa Sh6,800 miezi mitatu iliyopita na kuna hofu kwamba huenda bei ikashuka zaidi kufuatia kuwasili kwa nafaka za gharama nafuu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na mavuno ya mazao ya msimu mfupi ikiwa ni pamoja na maharage na viazi.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika mabohari ya NCPB katika kanda hiyo ulionyesha jinsi wakulima wamekuwa wakifika eneo hilo wakihofia kuuza mazao yao kwa bei ya hasara.

Bohari la NCPB Eldoret kwa mfano, linapokea kati ya magunia 5,000 hadi 8,000 ya mahindi kila siku huku wakulima wakitarajia kufaidika kutokana na bei bora na malipo ya haraka ya mazao hayo.

“Tumekuwa tukipokea maombi kutoka kwa wakulima walio tayari kuuza mazao kwa bodi kutokana na bei nzuri ikilinganishwa na soko la reja reja na malipo ya haraka-saa 24,” Gilbert Rotich meneja wa NCPB North Rift alisema.

Serikali inapanga kununua magunia milioni moja ya mahindi kwa Sh4,000 kwa gunia la kilo 90 kupitia NCPB kwa Hifadhi ya Kitaifa ya Kimkakati ya Chakula.

“Kufikia sasa tumenunua magunia 592,000 kati ya kilo 90 za mahindi lakini kuna ombi kutoka kwa wakulima walio tayari kupeleka mazao katika vituo vyetu ili wasipate hasara,” Titus Maiyo, meneja wa masuala ya ushirika wa NCPB alisema.

Wakulima wengi wakubwa katika eneo hilo wako mbioni kuuza mazao yao ili kuepuka kupata hasara kutokana na kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo.