Habari Mseto

Wakulima wang'oa michai kwa sababu ya bonasi duni

September 30th, 2019 1 min read

NA VITALIS KIMUTAI

WAKULIMA wa majani chai katika Kaunti ya Bomet wameanza kung’oa mimea hiyo kutokana na hasara waliyopata kutoka kwa Mamlaka ya Kilimo cha Majani Chai (KTDA) inayonunua mazao yao kwa bei duni.

KTDA imekuwa ikiwalipa wakulima bonasi ya chini hali ambayo imeibua hasira kutoka kwa wakulima wengi ambao sasa wanapania kushiriki kilimo cha mimea mingine ili kuongeza mapato yao.

Wakiwa na mashine za kukata miti, wakulima walifyeka michai na kuapa kuanzisha kilimo cha parachichi, kabeji, nyanya, viazi vitamu na maharagwe.

Hatua yao inajiri baada ya wakulima wanaowasilisha majani chai katika kiwanda cha Tegat kwenye Kaunti jirani ya Kericho kulalamikia kupungua kwa bonasi.

Kulingana na mkulima maarufu wa majani chai Richard Yegon kutoka Kipyosit, Bomet Mashariki, hasara wanayopata ni ya kiwango cha juu na hakuna haja ya kuendelea kushiriki kilimo kisichowanufaisha kwa vyovyote.

Bw Yegon aliwaongoza wakulima wenzake kung’oa michai shambani licha ya kushiriki kilimo hicho kwa miaka 15.

Mkurugenzi wa kiwanda cha majani chai cha Kapkoros Baxton Sigilai hata hivyo aliwaomba wakulima wakome kung’oa mihai yao akisisitiza kuwa mapato ya chini yanawaathiri hata wakulima kutoka maeneo mengine nchini.