Habari

Wakulima wataka ripoti ya jopokazi la sukari iwekwe wazi

July 30th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

WAKULIMA wa miwa katika Kaunti ya Kakamega wanataka ripoti ya jopokazi lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuchunguza changamoto zinazoikabili sekta ya sukari iwekwe wazi.

Jopokazi liliundwa Novemba 2018 liliongozwa chini ya uenyekiti wa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri akisaidiana na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya.

Mkulima wa kutoka Mumias Mashariki, Bw Justin Mutobera, na Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kitaifa la Wakulima wa Miwa Bw Simon Wesechere walisema matokeo ya ripoti hiyo iliyozingatia ukusanyaji wa maoni yanafaa kuwekwa wazi.

Wakiongea katika vikao tofauti, wakulima walilaumu jopokazi lililoongozwa na Kiunjuri kwa kuchelewesha ripoti.

“Tulitarajia ripoti ingekuwa tayari baada ya kipindi cha miezi sita, lakini sasa yaelekea kukamilika mwaka mmoja na hakuna chochote,” alisema Mutobera.

Mkulima huyo amemtaka Rais Kenyatta kuwasukuma Kiunjuri na Oparanya kuiweka wazi ripoti hiyo.

Bw Wesechere naye anashangaa ni kwa nini wanachama wa jopokazi na serikali imesalia kimya kuihusu ripoti hiyo ambayo huenda ikawa na mapendekezo muhimu ya kuifufua sekta ya sukari nchini.

“Kucheleweshwa kwa ripoti hiyo kutaathiri mikakati ya kuimarisha sekta hii,” alisema Wesechere.

Mei 2019, Bw Oparanya aliunda jopokazi lingine kujikita kwa mikakati ya kufufua kiwanda cha Sukari cha Mumias.

Ilitarajiwa kwamba baada ya majuma mawili ripoti ingekuwa tayari, lakini sasa yakaribia miezi minne.