Wakulima wataka Ruto atimize ahadi ya mradi wa Bura

Wakulima wataka Ruto atimize ahadi ya mradi wa Bura

NA STEPHEN ODUOR

WAKULIMA wanaotegemea mpango wa unyunyiziaji maji wa Bura, katika Kaunti ya Tana River, wametoa wito kwa serikali ya Rais William Ruto, kutimiza ahadi ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa mabomba mapya ya unyunyiziaji uliokwama kwa takriban miaka kumi sasa.

Wakulima hao wanakadiria hasara baada ya mashamba yao kukosa maji ya kutosha kwa miezi mitatu sasa, hali ambayo wataalamu wanasema inaweza tu kurekebishwa kupitia kwa mabomba mapya.

Mpango wa kujenga mabomba hayo yatakayosambaza maji kutoka milimani kuelekea nyanda za chini bila kutegemea kawi kwa takriban Sh7.1 bilioni, umekuwa ukibadilishiwa wanakandarasi mara kwa mara.

Akifanya kampeni eneo hilo Agosti, Rais Ruto aliahidi kwamba, kama angelishinda urais, serikali ingetafuta mkandarasi mpya kukamilisha mradi huo.

Kulingana na wakulima, huenda wakakosa mavuno mwaka huu kwa vile mimea yao imekauka na kuwaacha mashakani.

“Tulikuwa tumeweka matumaini yetu yote hapa. Akiba zetu zote za pesa tuliziweka katika mashamba yetu kwa matumaini ya kupata chakula, karo za watoto wetu na kupanua kilimo chetu. Angalia sasa…yote yamepotea,” akasema mkulima, Bw Francis Njenga.

Bw Njenga amedai kuna takriban ekari 300 za mashamba ambapo mimea imekauka, huku ekari nyingine 100 za mpunga zikielekea kunyauka.

Zaidi ya wakulima 100 wameathirika na kusababisha ukosefu wa ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 500 waliokuwa wakitegemea kazi na vibarua katika mashamba hayo.

Msimamizi wa mpango wa unyunyiziaji maji wa Bura, Bw Peter Orua, alisema mabomba yaliyopo kwa sasa hayawezi kutosheleza mahitaji ya wakulima wote hasa wale wa mpunga ambao mashamba yao huhitaji kiwango kikubwa mno cha maji.

Kulingana naye, wamelazimika wawe wakipiga maji kwa mgao ili wakulima wote wayapate kwa usawa.

“Kiufundi, mabomba yaliyowekwa hapa yalinuiwa kwa kilimo cha pamba na mahindi lakini sasa kuna sehemu kubwakubwa zinazopandiwa mpunga ambao unahitaji maji mengi. Mabomba hayawezi kustahimili mahitaji hayo kwa hivyo tunalazimika kugawa maji kila siku,” akasema.

Alieleza kuwa, walishauri baadhi ya wakulima wasipande mimea kwa sasa lakini wengine wakapuuza.

“Mpunga hutaka maji mengi mno. Tunapopiga maji asubuhi, ikifika mchana yashakauka katika mashamba ya mpunga. Hili ni jambo la kimazingira ambalo limetuzidi,” akasema.

Hata hivyo, wakulima wengine walidai kuwa changamoto za maji zinazowakumba zinasababishwa na ugavi wa maji kwa njia ambazo si za haki.

Wamedai kuna wakulima ambao hupokea maji mengi kuliko wengine, madai ambayo wasimamizi wa unyunyiziaji wameyakanusha.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona wapepeta Mallorca na kuendeleza presha kwa Real...

Kaunti kuboresha barabara zinazoelekea kwa mbuga za wanyama...

T L