Habari Mseto

Wakulima watapeliwa mamilioni na watu waliojifanya kutoka UN

January 17th, 2019 2 min read

Na BARNABAS BII

Wakulima wa mahindi eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wamepoteza mamilioni ya fedha kupitia kwa walaghai waliofika eneo hilo kununua mahindi kwa mkopo na bei nzuri.

Walaghai hao walijifanya kutumwa na Shirika la Mpango wa Chakula Ulimwenguni (WFP) na mashirika mengine ya kutoa msaada wa kibinadamu. Waliondoka eneo hilo kabla ya kuwalipa wakulima waliokuwa wamewasilisha mahindi yao.

Maafisa wa usalama eneo hilo jana walimkamata mshukiwa mkuu katika sakata hiyo baada ya wakulima kuandamana Kaunti ya Uasin Gishu, ambao walipoteza karibu magunia milioni moja katika sakata hiyo.

Mshukiwa huyo, Kairo Nyinya Sammy alikamatwa baada ya kuwapora katika eneo la Ziwa, Kaunti Ndogo ya Eldoret Magharibi kwa kununua magunia 700 kwa Sh3, 000 kwa kilo 90 ikilinganishwa na Sh1, 600 zinazotolewa na wasagaji wa kibinafsi.

Polisi walipata kitambulisho feki cha kidiplomasia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa na stakabadhi nyingine zilizotumiwa kuwaibia wakulima.

“Waporaji hao wanawadhulumu wakulima waliokata tamaa kwa kuwanunulia mazao yao kwa mikopo na kuwadanganya kuwapa Sh3, 000 kwa gunia. Wanajifanya wananunulia UN na kuwaahidi kuwalipa katika muda wa wiki moja,” alisema Zacharia Bitok, mkuu wa polisi wa Eldoret Magharibi.

Alisema washukiwa wengine watatu walikamatwa katika sakata hiyo ambayo inaaminika kuwapotezea wakulima mamilioni ya fedha.

Mmoja wa wakulima kutoka tarafa ya Moiben alipoteza magunia 200 na mwingine akapoteza magunia 100 kwa wafanyibiashara hao walaghai.

Chama cha wakulima (KFA) kimeonya wakulima kujihadhari sana na matapeli hao na kuwataka kuuzia Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB).

au wafanyibiashara wanaowaamini eneo hilo.

“Wakulima watapoteza zaidi ikiwa hawatauzia NCPB mazao yao au watengenezaji wa unga au wafanyibiashara wanaoweza kuaminika,” alisema mkurugenzi wa KFA Kipkorir Menjo.

NCPB inawapa wakulima Sh2, 500 kwa kilo 90 za mahindi baada ya agizo la Rais Uhuru Kenyatta wiki jana.

Watengenezaji huru wa unga wa mahindi wananunua mahindi kwa Sh1, 800 kwa gunia la kilo 90.

Matapeli hao watatu walikamatwa mwishoni mwa mwaka jana baada ya kumwibia mkulima Sh100, 000.

Baada ya kuwatapeli wakulima eneo moja, walaghai hao uhamia eneo lingine na kubadilisha nembo ya kazi ili kuwaibia wakulima zaidi.

Wakulima waliohojiwa walisema kucheleweshwa na NCPB kumewalazimisha kuuza mahindi yao kwa mawakala kwa bei ya chini sana kutokana na kuwa wanakabiliwa na changamoto za kifedha.