Habari Mseto

Wakunga wa kienyeji wataka kaunti iwalipe mshahara

August 8th, 2019 1 min read

Na KALUME KAZUNGU

WAKUNGA katika Kaunti ya Lamu wanaitaka serikali iwalipe mshahara kila mwezi kama njia ya kuwapa motisha wanapotekeleza shughuli zao za kila siku.

Wajuzi hao wa kuzalisha wamekuwa kiungo muhimu, hasa katika kuwasaidia wajawazito kutoka vijiji ambako miundomsingi ya afya, ikiwemo hospitali na zahanati bado ni duni.

Vijiji ambavyo bado vinakumbwa na ukosefu wa huduma bora za afya, Kaunti ya Lamu ni pamoja na Basuba, Mangai, Mararani, Milimani, Kiangwe, Mkokoni, Kiunga, Ishakani, Kiwayu, Kizingitini, Tchundwa, Mbwajumwali, Myabogi na baadhi ya sehemu za Faza, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Katika mahojiano na wanahabari kwenye miji ya Faza, Kizingitini, Kiunga, Ishakani na Basuba, wakunga walieleza haja ya kaunti kuwatambua kwa kuwapa mshahara kwani ujuzi wao umekuwa msaada mkubwa kwa wajawazito ambao wengi wao hawapati huduma za hospitali.

Msemaji wa wakunga hao, Bi Shumi Mkung, 60, alilalamika kuwa, mara nyingi wamekuwa wakiacha shughuli zao na hata familia zao baada ya kuhitajika kuhudumia wajawazito.

Alisema mbali na kuhudumia wajawazito vijijini, wakunga hao pia wamekuwa wakilazimika kuambatana na wajawazito hadi hospitalini, ambapo hupiga kambi kwenye hospitali hizo hadi pale watakapojifungua.