Habari

Wakurugenzi wa bwawa la mauti wapata afueni

January 7th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imesitisha kushtakiwa na kusikizwa kwa kesi dhidi ya wakurugenzi wawili wa kampuni ya Kensalt Limited iliyostawisha bwawa la Solai, Kaunti ya Nakuru ambalo lilipasuka mwaka 2018 na kusababisha vifo vya watu 48 kwa ulaghai wa shamba lenye thamani ya Sh2 bilioni Nairobi.

Jaji Pauline Nyamweya alisitisha kushtakiwa kwa Mansukhulal Shantilal Patel, Perry Mansukh Kasangra na aliyekuwa Mbunge wa Baringo Kusini Lawi Kigen Kiplagat katika mahakama ya Makadara.

Patel, Kasangra, aliyekuwa Mbunge wa Baringo Kusini Lawi Kiplagat na mfanyabiashara Nairobi James Wainaina Ndung’u wanakabiliwa na shtaka la kufanya njama za kughushi hatimiliki za kipande cha ardhi cha aliyekuwa Mbunge wa Lamu Mashariki Abubakar Madhubuti kati ya 1985 na 1996.

Patel na Kasangra walishtakiwa kwa ulaghai huu lakini hawakufika kortini Jumatatu kama walivyoagizwa Desemba 23, 2019.

Walitakiwa wajibu mashtaka lakini wakili wao William Arusei alisema hawakufika kortini kwa vile kesi inayowakabili imepigwa breki.

Jaji Nyamweya aliamuru Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) asiwafungulie mashtaka Patel na Kasangra hadi kesi waliyowasilisha mahakama kuu isikizwe na kuamuliwa.

“Polisi wanatumia vibaya mamlaka yao kuwafungulia mashtaka Mabw Patel na Kasangra kwa ulaghai wa shamba la ekari 10 ilhali wanajua kuna kesi inayoendelea katika mahakama kuu,” alisema wakili William Arusei.

Bw Arusei alimweleza Jaji Nyamweya kwamba aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu marehemu John Onguto alikuwa ameamuru walalamishi wote kuhusu umiliki wa kipande hicho cha ardhi wasikistawishe hadi mmiliki halisi ajulikane.

Akiwasilisha ombi la kusitisha kesi hiyo mbele ya Bw Nyaga , Bw Arusei aliomba kesi hiyo itajwe Aprili 30, 2020 kubaini ikiwa mahakama kuu imetoa maagizo zaidi.

Lakini kiongozi wa mashtaka Bi Jackline Kisoo aliomba mahakama itoe kibali cha kuwatia nguvuni Patel na Kasangra akisema “ walikaidi agizo la kufika kortini Jumatatu.”

Bi Kisoo alimweleza Bw Nyaga kwamba Bw Arusei alikuwa ameahidi kuwafikisha wateja hao wake kortini jana alipoomba mahakama ifutilie kibali cha kuwatia nguvuni Desemba 23, 2019.

Wote wanne Patel , Kasangra , Kiplangat na James Wainaina Ng’ang’a wanakabiliwa na shtaka la kughushi hatimili ya shamba la kampuni ya Taufflus Manufacturers Limited yake aliyekuwa Mbunge wa Lamu Mashariki, marehemu Abubakar Madhubuti kati ya 1985 na 1996.

Shamba hilo liko katika eneo la Kia Ng’ombe Embakasi kaunti ya Nairobi.

Lawi na Wainaina walikuwa mahakamani Jumatatu.

Bw Nyaga atatoa uamuzi iwapo atatoa kibali cha kuwatia nguvuni wawili hao Januari 13, 2020.