Habari Mseto

Wakurugenzi wa Platinum Distillers washtakiwa kukwepa kulipa ushuru

March 18th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAKURUGENZI wanne wa kampuni inayotengeneza mvinyo mjini Ruiru, Kiambu iliyofungwa Februari wameshtakiwa kwa kukwepa kulipa ushuru wa Sh41 milioni.

Mabw John Waweru Ndegwa, Onesmus Muturi Mburu, Michael King’ara na Bi Mary Wanjiku walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu Bi Roseline Oganyo Jumatatu.

Walikanusha shtaka la kukwepa kulipa ushuru wa malighafi ya kutengeneza mvinyo wa Ethanol kutoka India.

Washtakiwa hao walikanusha kati ya Februari 12 na 23 mwaka huu waliigiza nchini Ethanol ya lita 4,000 kinyume cha sheria za forodha za muungano wa mataifa ya afrika mashariki EACCMA nambari 157.

Mahakama ilifahamishwa Ethanol ingelilipiwa ushuru wa Sh41 milioni.

Lakini washtakiwa walipinga wakisema kila lita ya Ethanol hulipiwa ushuru wa Sh210.

“Ushuru ambao tungelilipa mheshimiwa ni Sh8 milioni na wala sio Sh4 1milioni,” wakili Mwihaki Igoro anayewatetea washtakiwa alimweleza hakimu.

Wakili wa aliyewakilisha washtakiwa Joshua Igoro. Picha/ Richard Munguti

“Wakati wa kusikizwa kwa kesi hii tutawasilisha ushahidi kuonyesha kuwa ushuru ambao tungelililipia ni Sh8milioni na wala sio Sh41 milioni. Pesa hizi za ziada wanazodai ni za kupeleka wapi?” aliuliza Bi Igoro.

Mahakama ilielezwa na wakili wa mamlaka ya ushuru nchini KRA Bi Nelly Ngovi kuwa dhamana inapasa kuwa sawa na kiwango cha ushuru wanachodaiwa washtakiwa.

 

Wakurugenzi hao walishtakiwa siku moja baada ya Jaji Weldon Korir wa Mahakama Kuu kukataa kuamuru KRA ifungue kiwanda cha Platinum Distillers Ltd na mabohari ya Multiplan Packaging Ltd ambapo Ethanol hiyo inahifadfhiwa.

Kiwanda hicho kilifungwa wakati wa operesheni iliyoongozwa na aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) aliyestaafu mapema wiki hii Bw Joseph Boinnet na Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai George Kinoti.

Jaji Korir alisema KRA ilifunga kiwanda hicho ifanye uchunguzi kubaini ikiwa Ethanol hiyo iko na madhara kwa afya ya binadamu.

Wakili wa KRA Bi Nelly Ngovi. Picha/ Richard Munguti

Katika kesi hiyo ya Platinum mahakama kuu , wakili Chris Kabugu aliyeiwakilisha aliieleza mahakama maafisa wa KRA pamoja na wakuu wa Polisi walikifunga kiwanda hicho na kulemaza oparesheni zake kabisa.

“Haki za kufanyakazi na kumiliki mali zinazofurahiwa na wakenya kwa mujibu wa katiba zilikandamizwa na maafisa wa KRA waliovamia kiwanda hicho mjini Ruiru wakidai kumeigizwa kemikali ya sumu Ethanol,” alisema Bw Kabugu.

Katika uamuzi wake Jaji Korir alikubalia KRA kuchunguza Ethanol hiyo kwa siku 30 na kuamuru iwakubalie wakurugenzi hao kuendelea na shughuli zao.

Hakimu aliamuru kila mmoja washtakiwa hao alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000.

Kesi itatajwa baada ya siku 14.