Habari Mseto

Wakurugenzi wanaopokea mshahara mara 50 ya wafanyakazi

June 21st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wakurugenzi wakuu wa benki kubwa nchini hupokea mshahara mkubwa zaidi kuliko wafanyikazi wa benki hizo.

Kulingana na ripoti iliyotolewa, wakurugenzi hao hupokea mara 50 ya mshahara ya wafanyikazi wao.

Habari hiyo kutokana na utafiti inaonyesha tofauti kubwa sana ya kimapato kati ya wakurugenzi na wafanyikazi wao katika sekta ya kibinafsi.

Kulingana na data hiyo, wakurugenzi wa benki mwaka jana walipata Sh128.3 milioni, mshahara wastani.

Kati ya benki zilizotafitiwa ni KCB, Equity na Co-op bank. Mkurugenzi Mkuu wa Co-op Bank, Gideon Muriuki ndiye alipata mshahara mkubwa zaidi(370.5 milioni) na kufuatwa na Mkurugenzi Mkuu wa KCB, Joshua Oigara, aliyepokea Sh256 milioni kwa mwaka.

James Mwangi wa Equity alipokea Sh60.4 milioni mwaka huo na kufuatwa na Mkurugenzi Mkuu wa National Bank of Kenya (NBK)  ambapo alipata Sh48 milioni.

Wafanyikazi wa Stanbic ndio hulipwa mshahara wa juu zaidi, wa Sh446,666 kwa mwezi.

Kati ya benki kubwa, ni benki ya Barclays ambayo imeonekana kusawazisha mishahara kati ya wakurugenzi na wafanyikazi kwa kiwango fulani, ambapo kiwango cha wastani cha mshahara wa wafanyikazi wake kilikuwa ni Sh373,676 na kufuatwa na Standard Chartered Bank ambapo kiwango hicho kilikuwa ni Sh363,275.