Habari Mseto

Wakurugenzi kizimbani kwa ulaghai wa shamba la Sh54 bilioni

January 14th, 2019 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

WAKURUGENZI wawili wa kampuni ya ununuzi wa mashamba walishtakiwa kupokea mamilioni ya pesa wakidanganya watawauzia vipande vya ardhi katika shamba kubwa la kibinafsi la Kapiti Plains Estate Limited lenye thamani ya Sh54.8 bilioni.

Bw Muthiani Mwangangi mwenye umri wa miaka  42 alishtakiwa pamoja na mkurugenzi mwenzake Bi Eveline Mbithe mwenye umri wa miaka 57.

Bw Mwangangi na Bi Mbithe ni wakurugenzi katika kampuni ya New Konza South Ranch Limited lenye afisi zake katika mji wa Chumbi ulio kwenye makutano ya barabara za Machakos na Mombasa.

Wawili hao walikabiliwa na mashtaka 10 ya kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu na kufanya njama za kuilaghai kampuni ya Kapiti Plains Estate Limited shamba lake la zaidi ya ekari 100,000.

Katika shtaka la kwanza wakurugenzi hao wanadaiwa kati ya Januari 20, 2017 wakishirikiana na watu wengine wanaoendelea kusakwa na Polisi walifanya njama kutapeli kampuni ya Kapiti Plains Estate Limited shamba lake lililo na thamani ya Sh54,800,000,000.,

Wawili hao walikabiliwa na shtaka la pili la kughushi hati ya umiliki wa shamba hilo la Kapiti mnamo Septemba 28, 2010.

Cheti hicho feki cha kujipatia shamba hilo la Kapiti kilikuwa kimeandikwa kilitayarishwa mnamo Agosti 23 1994 kwa jina la New Konza Ranch Association.

Wawili hao walidai hati miliki hiyo ilikuwa imetolewa na kutiwa saini na Kamishna wa Ardhi.

Kwa hatia za kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu wawili hao walidaiwa mnamo Julai 29,2013 walipokea Sh100,000 kutoka kwa Bw Michael Kivuvo wakidai wangelimuuzia ardhi katika shamba hilo la feki.

Walikuwa wamempa Bw Kivuvo ploti nambari 7 katika shamba hilo nambari ya usajili Konza South/Konza South Block4/1482 wakijua wamemdanganya au kumlaghai.

Shtaka la nne lilisema walipokea Sh350,000 kutoka kwa Bi Veronica Mwikali Kuyumya. Pesa hizi zilikuwa za ploti mbili nambari 3 na 13 katika shamba hilo.

Walidaiwa walijua wanamfuja Mwikali.

Wengine walioporwa ni Mabw Anselem Makau Mutisha Sh100,000, Machariah Karanja Sh100,000 , Muthusi Mulei Sh200,000, James Kariuki na Lydia Wangari Muchai Sh200,000 na Ezekiel Musau Mulwa Sh100,000.

Wakili Francis Kalwa anayewatetea washukiwa hao alimweleza hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot kwamba Bw Mwangangi anaugua kisukari na bintiye Deborah Muthiani anaugua Asthma.

“Washtakiwa hawa wanaugua maradhi ya Asthma. Hawataroka hata wakiachiliwa kwa dhamana,” alisema Bw Kalwa.

Mahakama iliwaachilia kwa dhamana ya Sh300,000 pesa tasilimu.

Kesi itaanza kusikizwa Februari 2, 2019.