Wakuu wa Bhadala Jamat walaani vurugu zilizotokea katika makao makuu

Wakuu wa Bhadala Jamat walaani vurugu zilizotokea katika makao makuu

NA JURGEN NAMBEKA

WAKUU wa muungano wa Waislamu wa Bhadala Jamat (BJM) kutoka Mombasa, Jumatano wamelaani vurugu zilizotokea katika makao yao makuu, wakidai zilisababishwa na watu waliotaka kuharibu jina la BJM.

Akizungumza katika makao makuu ya BJM, msemaji wa jamii hiyo yenye wanachama takriban 3,000 kote nchini Bw Tarmuhamed Kana alieleza kuwa, watu ambao hawahusishwi na jamii hiyo walitumiwa kuleta vurugu kwa manufaa ya mtu mmoja.

Anahoji kuwa, baada ya mmoja wao Bw Jaffah Soda kushindwa katika uchaguzi wao wa mwisho mnamo 2014, amekuwa akipinga maendeleo ya jamii hiyo kupitia jamaa zake.

Uchaguzi huo ambao haujafanyika kwa miaka minane sasa, ulikuwa ufanyike kabla ya watu hao kuleta vurugu iliyosababisha watu kadhaa kujeruhiwa.

“Jamaa mmoja anayeitwa Bw Japhah Sodah ambaye alishindwa katika kura mnamo 2014, ndiye tunaamini aliwaleta hao watu kusababisha vurugu. Tulishtukia tu watu wamejikusanya nje ya lango kuu ya makaazi haya, na mwishowe wakatumia nguvu na kuingia humu ndani,” alisema Bw Kana.

Uchaguzi huo ambao wapaswa kufanyika kila baada ya miaka minne, haujakuwa ukifanyika kwasabu ya kesi iliyosajiliwa mwaka 2018 kusimamisha mkutano wa mwaka huo. Mkutano huo ulifanya kiongozi wa 2018 asichaguliwe.

Kulingana na Bw Kana, watu hawa wanaotokea kwenye ukoo wa Garana, ambayo si moja ya koo zilizo katika jamii ya BJM, walitaka wahusishwe na shughuli za jamii hiyo licha ya kutokuwa wanachama.

Walieleza kuwa watu hao waliotaka kuhusishwa na BJM, hawakufuata sheria ya kujisajili kuwa wanachama.

“Kama jamii tuna mahitaji ya kuwa mwanachama. Kwanza, ni lazima utume ombi. Iwapo uongozi wa jamii ya BJM itakukubali, basi utaulizwa ujiunge na ulipe kodi ya Sh 500 kila mwaka. Waliokuja kuzua vurugu sio wanachama wetu na hawana vibali,” alisema Bw Kana.

Bw Kana alieleza kuwa, huenda watu hao walidhania ni wanachama kwa sababu ya kukubaliwa washiriki katika sikukuu zote za kiislamu.

Mmoja wa wawaniaji wa uwenyekiti wa jamii hiyo Bw Abdulkarim Yusuf Jetwa, alieleza kuwa waliotaka kuhusishwa hawatoki kwenye koo 32 za Bhadala.

“Sisi Wabhadala kulingana na historia tulikuwa wa kwanza kukita kambi hapa Kenya. Hawa Wagarana wanaotufuata, walikuwa wakimbizi tuliowasaidia hapo awali. Wanaotaka kuhusishwa na sisi hawajawahi kuwa wetu. Hata katika koo zetu 32 hawapo. Hawachangii chochote katika jamii yetu,” alisema Bw Jetwa.

Vurugu hizi zilishuhudiwa baada ya sehemu ya watu, waliojitokeza kuhudhuria mkutano kudai kuwa, walikuwa wamezuiliwa kuingia katika mkutano wa Jumapili.

Kundi hili la watu lilidai kuwa, lilikuwa na haki ya kushiriki uchaguzi huo na lilikuwa limetengwa. Walitaka wahusishwe katika shughuli ya kupiga kura kwa nguvu na hapo ndipo vita vikazuka.

Vita hivi vilikuwa kati ya Wabhadala na hao waliodai kuwa sehemu ya jamii ya BJM, licha ya kukanwa na jamii hiyo.

Mwakilishi wao alilalamikia kuzuiwa kupiga kura akisema kuwa, waliokuwa kwenye hatamu hawakutaka kuondoka uongozini, ukoo mwingine uingie.

Uongozi wa BJM ulieleza kuwa ulilaani vurugu hizo wakieleza kuwa, wao ni watu wenye kupenda amani, demokrasia na sio vita.

  • Tags

You can share this post!

Jaji Mkuu Martha Koome ateua majaji 3 kusikiliza kesi ya...

Polisi wakamata washukiwa 81 na kutwaa silaha hatari Mtwapa

T L