Wakuu wa kaunti washtakiwa kwa wizi wa Sh17.9 milioni

Wakuu wa kaunti washtakiwa kwa wizi wa Sh17.9 milioni

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA afisa mkuu idara ya fedha katika Kaunti ya Nairobi Jimmy Kiamba aliyefungwa miaka 12 pamoja na maafisa wengine wakuu wanne Jumatatu walipatikana na hatia ya kuilaghai kaunti Sh17.9 milioni.

Kiamba na wenzake hao walikuwa maafisa wakuu katika serikali ya aliyekuwa Gavana Dkt Evans Kidero.

Kesi iliyowakabili watano hao ilisikilizwa na hakimu mkuu Kennedy Bidali na kuwaachilia.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alikata rufaa iliyosikilizwa na Jaji Esther Maina na kubatilisha uamuzi wa Bw Bidali na kuwafunga jela washtakiwa miaka 12.

Na wakati huo huo Jaji Maina aliwaamuru watano hao wafike mbele ya hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Lawrence Mugambi kujitetea katika kesi ya ulaghai wa Sh17.9milioni.

Kufuatia uamuzi huu hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Lawrence Mugambi aliwaamuru wafungwa hao waanze kujitetea Oktoba 5, 2022 kabla ya uamuzi kutolewa.

Kiamba ameshtakiwa pamoja na Reginah Chepkemboi Rotich, Stephen Ogaga Osiro, Lilian Wanjiru Ndegwa na Nancy Waithera Kiruri.

Wote watano walishtakiwa kwa kula njama za kuilaghai NCC.

Wafungwa hao watano walimweleza hakimu watawaita mashahidi 24 watakapoanza kujitetea.

Watano hao walikabiliwa na shtaka la kula njama za kuilaghai kaunti ya Nairobi Sh17,902,728 kati ya  Novemba 1, 2013 na Aprili 3, 2014.

Mbali na kesi hiyo Kiamba, Ndegwa na Osiro wanabakiliwa na kesi nyingine pamoja na Kidero ya ulaghai wa Sh213 milioni.

Mahakama ilifahamisha Rotich kulipa faini ya Sh1.2 milioni aliyotozwa na Jaji Maina. Anatumikia kifungo katika gereza la wanawake la Lang’ata.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke amtuza Rais Kenyatta batamzinga 10 kwa kutengeneza...

Warembo wa Brazil wazamisha Colombia na kutawazwa malkia wa...

T L