Kimataifa

Wakuu wa maandamano wadai serikali inawawinda

October 24th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

ABUJA, Nigeria

VIONGOZI wa maandamano ya kulalamikia ukatili wa maafisa wa polisi nchini Nigeria, wamehimiza raia kukaa nyumbani baada ya kudokezewa habari kwamba wanawindwa.

Kupitia muungano wao wa Feminist Coalition ambao umeandaa maandamano hayo ya wiki tatu sasa, wameshauri watu kufuata kafyu zozote katika majimbo yao.

Hatua ya waandalizi hao inajiri baada ya habari kwamba wanachama wa muungano huo wanatishiwa maisha.

Barabara za jiji kuu Lagos, ambalo limekuwa kitovu cha maandamano hayo, zilikuwa tulivu Alhamisi usiku lakini hofu bado ilikuwa imetanda.

Majumba katika jiji hilo na miji mingine yalichomwa, maduka kuporwa na magereza kuvamiwa tangu Jumanne usiku waandamanaji walipofyatuliwa risasi jijini Lagos.

Shirika la kutetea haki la Amnesty International lilisema kwamba maafisa wa usalama waliwaua watu 12, ingawa jeshi la Nigeria limekanusha kuhusika katika mauaji yoyote.

Maandamano yalianza wiki tatu zilizopita wananchi, hasa vijana, wakitaka kikosi hatari cha polisi cha kukabiliana na unyang’anyi kivunjwe.

Kikosi hicho maarufu kama Special Anti-Robbery Squad (SARS) hatimaye kilivunjwa mnamo Oktoba 11.

Waandamanaji pia walidai kuwa wanajeshi waliwafyatulia risasi ili kuwaua.

Rais Muhammadu Buhari katika hotuba ya televisheni alilitaka jeshi kutekeleza majukumu yakee kwa kuzingatia sheria.

Katika hotuba hiyo Alhamisi usiku, Buhari pia alihimiza waandamanaji kusitisha maandamano na kufanya mazungumzo na serikali ili kutafuta suluhu.

Hata hivyo, hakuzungumzia hususan mauaji ya waandamanaji yanayodaiwa kufanywa na maafisa wa usalama, ambayo yameshutumiwa kote ulimwenguni.

Hotuba ya Buhari ilikosolewa mno katika mitandao ya kijamii ambapo vuguvugu la #EndSars liliasisiwa. Wengi walisema hakushughulikia matakwa ya waandamanaji. Badala yake alitilia mkazo kauli za vijana wengi wa Nigeria kwamba wanalengwa na serikali kupitia maafisa wa usalama.

Kwenye taarifa waliyochapisha kwenye mtandao wa Twitter, waandalizi wa maandamano hayo, ambao wamekuwa wakitumia hashtegi #EndSars, walilaani ghasia zote zilizotokea wakisema “vijana wa Nigeria wanahitaji kuendelea kuwa hai ili kutimiza ndoto ya kujenga nchi yao siku zijazo.”

“Sisi ndio wajumbe wa matumaini. Lengo letu wakati wote ni maslahi na usalama wa vijana wa Nigeria,” ilisema taarifa hiyo.

Iliongeza: “Kufuatia hotuba ya rais, tunahimiza vijana wote kutulia, kukaa nyumbani na kutii kafyu katika majimbo yao.”

Vile vile, kundi ilo lilisema halitapokea tena michango ya pesa lakini litatumia Sh3.6 milioni kutoka kwa wafadhili kuwasaidia wake ng’ambo kulipia waathiriwa wa ukatili wa polisi bili za hospitali na ada za mawakili. Makundi mengine na watu maarufu pia wamekuwa wakipanga maandamano na haikubainika iwapo yatafuata mkondo wa The Feminist Coalition.