Habari Mseto

Wakuu wa Oil Libya wakana kuiba Sh1.5m

June 5th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu iliamuru wafanyakazi wakuu watano wa kampuni ya kuuza mafuta ya  Oil Libya Kenya Limited washtakiwe kwa kosa la kuvunja na kuiba mali yenye thamani ya Sh1.5 milioni.

Jaji Enock Chacha Mwita aliamuru Joyce Nekoye Wanjala, Nancy Waeni Mutune Kwinga, Antony Mugo, Stanely Njoroge na raia wa Zimbambwe Duncan Ziyani Murashiki Thomas washtakiwe kwa kuvunja na kuiba kutoka kituo cha kuuza mafuta cha Juja Service Station kinachomilikiwa na kampuni ya Maced Ltd.

Baada ya juhudi za washukiwa hao kuzima hatua ya kushtakiwa kugonga mwamba walijisalamisha mbele ya hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot kusomewa mashtaka.

Walikanusha walivunja na kuiba kutoka kwa kituo cha mafuta cha Juja Service Station mali yenye thamani ya Sh1.5milioni.

Walikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh100,000.

Kampuni ya Maced ilipinga hatua ya washtakiwa hao kupinga wakijibu mashtaka na kusema kuwa “ wakuu hao wa Oilibya walikuwa wakiishurutisha kusitisha mkataba wa kibiashara.”

Mahakama ilifahamishwa na Maced kuwa kuna kipengee katika mkataba wao kwamba lazima arifa itolewe kabla ya kutamatisha kandarasi kati yake na Oilibya.

Wakili James Ochieng Oduol anayewatetea washukiwa awasilisha ombi la dhamana. Picha/RICHARD MUNGUTI

Walipovunja kituo hicho na kuiba kamera za CCTV na bidhaa za mafuta walikodisha mfanya biashara mwingine kituo hicho cha kuuza mafuta ya petrol.

Washtakiwa hao walipinga kushtakiwa kwao upya wakidai Machi 2019 mkurugenzi wa mashtaka ya Umma (DPP) alitamatisha kesi sawa na hiyo dhidi yao na “ kushtakiwa kwao tena ni kukandamiza haki zao.”

Washtakwa hawa walikuwa wamesema wanadhulumiwa kwa kushtakiwa tena.

Lakini Jaji Mwita akasema kuwa ijapokuwa walikuwa wameachiliwa , kifungu cha sheria nambari 87 (a) kilichotegemewa kuachiliwa nyakati za aliyekuwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Keriako Tobiko ambaye sasa ni Waziri wa Mazingira kimetoa fursa ya kukamatwa na kushtakiwa tena.

Maced ilimwandikia DPP wa sasa Noordin Haji na kulalamika haikupata haki kwa vile bidhaa zake ziliibwa na washtakiwa na walipoteza biashara.

Maced ilikuwa pia imewasilisha kesi katika kitengo cha biashara na kushtaki ilipwe fidia na Oilibya kwa kuvunja mkataba wa kibiashara.

Washtakiwa walipinga wakishtakiwa upya wakisema kuna kesi ya kibiashara lakini mahakama ikasema kifungu nambari 134 kinaruhusu kesi mbili kuendelea.

“Kuwapo kwa kesi nyingine sio kizingiti cha kutowashtaki kwa uhalifu wafanyakazi hawa wanaodaiwa walivunja na kuiba,” alisema Jaji Mwita akiamuru DPP aendelee na kesi dhidi ya watano hao.

Bw Cheruiyot aliwaachilia kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu washtakiwa hawa na kuamuru kesi isikizwe Septemba 18, 2019