Habari Mseto

Wakuzaji kahawa Kirinyaga kufaidi ushirikiano na India

January 15th, 2020 1 min read

Na GEORGE MUNENE

WAKULIMA wa kahawa wanatarajiwa kupata faida iwapo ushirikiano kati ya serikali ya kaunti ya Kirinyaga na wanunuzi kutoka India utafanikishwa.

Kwa miaka mingi wakulima wamekuwa wakichuma mapato duni kutokana na mauzo ya zao hilo lakini sasa utawala wa Anne Waiguru umejitolea kupata soko bora kwa zao hilo.

Viwanda vya kusaga kahawa katika eneo hilo hununua kahawa kwa Sh56 kwa kilo ya kawaha inayowasilishwa, bei ambayo wakulima wamekuwa wakilalamika kwamba ni duni mno.

Wakulima wamekuwa wakiishinikiza serikali ya kaunti kuingilia kati kuhakikisha kuwa wanalipwa Sh100 kwa kilo ya zao hilo ili wafaidi kwa sababu kilimo kimegatuliwa.

Hii ndiyo maana Gavana Waiguru ameanzisha mazungumzo kati ya serikali yake na wawekezaji ambao wameelezea nia ya kununua kahawa. Vile vile, amekuwa akifanya mazungumzo na wasimamizi wa vyama 15 vya ushirika kutoka eneo la Mlima Kenya kwa lengo la kuimarisha bei ya zao.

Mmoja wa wawekezaji hao, Nihar Gupta, alisema mazungumzo hayo yanaendelea vizuri.

“Mazungumzo yetu yanaendelea vizuri na tunalenga kuhakikisha kuwa wakilima wa kahawa Kirinyaga wanapata soko nzuri, ya kutegemewa na itakayowafaidi,” akasema, kauli ambayo iliungwa mkono na Gavana Waiguru.

Wawekezaji hao kutoka India ambao ni wanachama wa kampuni ya SPG group of Companies, watarajiwa kuanza kununua kahawa baada ya makubaliano kuafikiwa.

Gavana Waiguru alifafanua kuwa serikali yake itahakikisha wakulima wanauza kahawa yao kwa mkataba wa miaka 10 ambapo watahakikishiwa mapato ya kudumu.

Alisema wakulima ambao wakati huu wametia saini kandarasi kati yao na viwanda kwa kahawa pia watahakikishiwa mapato ya maalum kuanzia mwaka wa kifedha ujao.

“Chini ya mpango kama huu wakulima wakulima ambao wamekuwa wakipata mapato duni kwa miaka mingi watapata afueni kubwa,” akasema Bi Waiguru.