Wakuzaji minazi nao walilia fidia

Wakuzaji minazi nao walilia fidia

NA MAUREEN ONGALA

WAKULIMA wa minazi katika Kaunti ya Kilifi, wamelalamikia kutengwa na serikali wakati wanapoendelea kukosa mazao kwa mwaka wa tano wa kiangazi kikali.

Wakulima hao ambao wengi ni kutoka Rabai wamesema wamejipata kwenye umaskini huku gharama ya maisha ikizidi kupanda.

Mmoja wao, Bw Nzaka Mwotovu, alisema changamoto ya kufufua kilimo cha minazi inasababishwa na ukosefu wa viongozi waliojitolea kusukuma ajenda hiyo serikalini kwa niaba ya wakulima.

Kulingana naye, viongozi wa kisiasa kutoka maeneo ya bara huwatetea vikali wakulima kama vile wa miwa, majanichai, mahindi na kahawa wakati kilimo cha mimea hiyo kinapokumbwa na changamoto, hadi serikali ya kitaifa huingilia kati, lakini hali sivyo kwa wakulima wa minazi Pwani.

“Hakuna kiongozi yeyote ambaye amejali kuwatafutia fidia wakulima wetu jinsi tunavyoona maeneo ya bara wakati mimea yao mikuu ya kilimo inapoathirika,” akasema Bw Mwotovu.

Katika maeneo ya Kaloleni na Watamu, Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini, baadhi ya wakulima waliamua kuwekeza kwa unyunyizaji maji katika mashamba yao ya minazi.

Bw Baha Nguma akiwapa mbegu za mnazi wakulima katika kijiji cha Mbarakachembe wadi ya Watamu katika eneobunge la Kilifi Kaskazini, Kaunti ya Kilifi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Bw Christopher Kitsao kutoka kijiji cha Mbarakachembe, Watamu, alisema walikadiria kuwa wangepata hasara kubwa zaidi kama mimea yote ingekauka ndipo wakaamua kutafuta maji ya kunyunyizia minazi iliyobaki.

“Tayari tulipata hasara lakini wengine wetu hatukutaka kuacha kilimo cha minazi kwa sababu ya kiangazi, tukaamua kunyunyizia maji ile mimea iliyobaki,” akasema.

Mbunge wa Rabai, Bw Kenga Mupe, alisema atawasilisha hoja bungeni ili serikali ishurutishwe kuwalipa fidia wakulima wa minazi ili wapate namna ya kujitegemea.

Akizungumza katika eneo la Shika Adabu, Wadi ya Rabai/Kisuritini, Bw Mupe alisema licha ya kuwa tegemeo kubwa la kiuchumi, kilimo hicho kimepata pigo katika miaka iliyopita kwa sababu ya kiangazi na minazi mingi imekauka huku mingine ikikosa kutoa mavuno.

“Sote tunajua kumekuwa na ukame na hali hii bado inaendelea. Jami imekuwa ikitegemea kilimo cha minazi lakini mimea mingi imekauka na watu wamepoteza mbinu za kujichumia riziki na sasa wanataabika kimaisha,” akasema.

Mbali na hayo, mbunge huyo alisema atashauriana na serikali nyingine za kaunti na mashirika ya kimaendeleo ili kutafuta mbinu ya kuwezesha wakulima kupata mazao bora na kuongeza thamani ya mazao yao.

“Sisi kama viongozi wa kitaifa na wa kaunti, tumejitolea kuhakikisha kuna maendeleo katika maeneo yetu ili kuboresha maisha ya watu wetu,” akaeleza.

Bw Christopher Kitsao (kushoto), mkulima wa nazi kutoka kijiji cha Mbarakachembe wadi ya Watamu katika eneobunge la Kilifi Kaskazini akipokea ujuzi wa kutunza mnazi unaomea kutoka kwa aliyekuwa katibu mkuu wa kilimo kaunti ya Kilifi Bw Baha Nguma ambaye amejitolea kuwapa ushauri wakulima katika kijiji chake. PICHA | MAUREEN ONGALA
  • Tags

You can share this post!

Gavana Mwadime alenga utalii kuinua uchumi wa Kaunti

Wakenya wavuma kwa wizi ng’ambo

T L