Habari Mseto

Wakuzaji miwa wakataa jopo la kufufua sekta

January 15th, 2019 1 min read

Na VICTOR RABALLA

WAKULIMA wa miwa wameilaumu serikali wakidai imewapuuza katika majadiliano yanayoendelea kuhusu namna ya kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo cha miwa.

Wakulima hao Jumatatu waliunda jopo walilolitwika jukumu la kuwasilisha mapendekezo yao kwa Rais Uhuru Kenyatta na wakaapa kwamba hawataruhusu kuingizwa kwa pendekezo la kila kampuni kupokea miwa kutoka kwa wakulima wa eneo lake pekee wakati wa kuidhinishwa kwa mapendekezo mapya ya kudhibiti sekta ya sukari.

Vile vile walimkashifu Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri kwa kuunda jopo la watu 16 bila kuwahusisha wakulima, ambao ni kiungo muhimu katika sekta ya kilimo cha miwa.

“Jopo lililoundwa halina umuhimu. Hakuna vile serikali inaweza kujizungumzia, kujichunguza kisha kujiandalia mapendekezo,” akasema Mwekahazina wa Chama cha Kitaifa cha Wakulima wa Miwa (KNFSF), Bw Stephen Narupa.

Wakulima hao waliowasilisha matakwa yao kwa ofisi ya Gavana wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o, walimteua mwenyekiti wa zamani wa iliyokuwa bodi ya sukari ya Kenya, Saulo Busolo kama atakayeyawasilisha malalamishi yao kwa Rais Kenyatta.

“Tumeamua kubuni jopo linaloongozwa na wakulima kuhakikisha kwamba haki zao zinazingatiwa na tutawasilisha mapendekezo yetu kwa Rais Kenyatta kupitia kwa waziri katika muda wa siku 30 zijazo,” wakasema.

“Wakulima wana haki ya kuuza miwa yao kwa kampuni yoyote wanayotaka,” akasema Bw Narupa.

Naye Katibu wa Muungano wa kitaifa wa Wakulima wa Miwa (KESGA), Richard Ogendo alishutumu jopo lililoundwa la watu 16 kwa kukosa kuwaalika wawakilishi wa vyama vya wakulima wa miwa na kutumia wawakilishi kutoka viwanda vya sukari kuficha ukweli.

Wakati huo huo, wakulima hao walimwomba Bw Kiunjuri kuharakisha malipo ya deni la Sh2.6 bilioni jinsi alivyoamrisha Rais Kenyatta mwaka uliopita.

Naibu Gavana wa Kisumu, Mathews Owili alipokea nakala ya ombi lao na kuwaahidi kwamba masuala waliyoyaibua yatashughulikwa vizuri.