Habari Mseto

'Walanguzi wa bangi, dawa za kulevya wapewe adhabu kali'

December 16th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

SHERIA kali inastahili kuchukuliwa dhidi ya walanguzi wa bangi na dawa za kulevya.

Kamanda mkuu wa polisi Thika Magharibi, Bi Beatrice Muraguri, alisema walanguzi wengi wanaonaswa na bangi na dawa za kulevya mara nyingi wanatozwa faini na wengine hata hupewa kifungo cha probesheni, huku wengine wakiagizwa kufanya kazi za kuitumikia jamii kwa muda.

“Mahakama zetu siku hizi zinatoa hukumu nyepesi ambazo watu wengi wana uwezo wa kutoa faini na kuachiliwa huru. Baadaye wanarejea tena kwa biashara hiyo. Ni sharti sheria kali iwekwe kwa walanguzi hao ili kupunguza tabia hiyo kuendelea,” alisema Bi Kiraguri.

Aliyasema hayo Jumatatu katika afisi yake akielezea jinsi hali hiyo inavyotatiza maafisa wengi wa polisi.

Alisema mahakimu wengine hata hutoza wahusika faini ya Sh20,000 pekee kwa walionaswa na dawa hizo, ambapo wanafanikiwa kulipa kwa urahisi.

Aliwashauri wazazi wawe makini kwa kufuatilia ni mambo yapi wana wao wanayafanya kila mara wakiwa mbali nao.

Alisema wamegundua ya kwamba walanguzi wa bangi na mihadarati iliyopakiwa kwa paketi ni vijana wa kati ya miaka 12 na 35.

Aliwataka polisi wasishirikiane na walanguzi hao kwa sababu iwapo yeyote atanaswa na madawa hayo bila shaka atashtakiwa kawaida kama mhalifu wa kawaida.

“Ninawashauri polisi popote walipo wazingatie kazi yao kwa unyenyekevu bila kuingia majaribioni,” alisema afisa huyo.

Mbunge wa Thika katika mahojiano hivi majuzi alisema sheria za dawa za kulevya zinastahili kufuatiliwa kikamilifu.

“Serikali inastahili kuhakikisha wale wanaopatikana na makosa wanaadhibiwa vilivyo bila huruma,” alisema.

Alisema iwapo mswada utapitishwa bungeni ni sharti sheria hiyo itekelezwe ipasavyo bila huruma.

“Mara nyingi kukosa kutekeleza sheria ipasavyo ndiko kunaleta shida katika sheria hiyo,” alisema Bw Wainaina.

Alitoa wito kwa vijana kujiepusha na ulanguzi wa dawa za kulevya kwa vile kunawapotosha katika maisha.

“Ninatoa wito kwa vijana wasikubali kupotoshwa ama kutumiwa na walanguzi kusambaza dawa hizo za kulevya,” alisema Bw Wainaina.

Alisema wakati huu wa likizo ni hatari sana kwa vijana na kwa hivyo wahakikishe wanafuatilia mienendo yao na marafiki wanaotembea nao.