Kimataifa

Walanguzi wote wa dawa za kulevya wanyongwe – Trump

March 21st, 2018 1 min read

Na AFP

RAIS Donald Trump wa Amerika sasa anataka walanguzi wa dawa za kulevya wanyongwe kama njia mojawapo ya kukabiliana na mihadarati nchini humo.

Rais Trump alizindua rasmi pendekezo hilo alipokuwa akihutubu katika eneo la Manchester jimboni New Hampshire.

“Walanguzi wa mihadarati ni watu wabaya na tunahitaji kuwachukulia hatua kali. Ikiwa tutawahurumia basi mihadarati itaendelea kutuathiri, wanyongwe,” akasema Rais Trump.

Jumla ya watu milioni 2.4 ni waraibu wa dawa za kulevya ambazo zinajumuisha heroini. Inakadiriwa kuwa dawa za kulevya huua watu 115 kwa siku, kulingana na takwimu za Idara ya Afya.

Rais Trump aliahidi kukabiliana na tatizo sugu la dawa za kulevya lakini kufikia sasa hajapiga hatua yoyote.

Kulingana na sheria mpya, watu wanaoua baada ya kutumia dawa za kulevya wanastahili kuhukumiwa adhabu ya kifo. Lakini kufikia sasa hakuna mshukiwa amehukumiwa kwa kutumia sheria hiyo.

Tafiti ambazo zimewahi kufanywa zinaonyesha kuwa, asilimia 55 ya Waamerika wanaunga mkono adhabu ya kifo dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya.