Michezo

Walcott arejea Southampton kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Everton

October 6th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

SOUTHAMPTON wamemsajili aliyekuwa mchezaji wao, Theo Walcott kwa mkopo wa kipindi cha mwaka mmoja kutoka Everton.

Walcott, 31, anajivunia kuchezea timu ya taifa ya Uingereza mara 47. Alianza kupiga soka yake kitaaluma akivalia jezi za Southampton kabla ya kujiunga na Arsenal mnamo 2006.

Everton walimtwaa kutoka Arsenal mnamo Januari 2018 kwa kima cha Sh2.8 bilioni.

“Nilikuwa na ofa nyinginezo kutoka kwa klabu mbalimbali za bara Ulaya. Hata hivyo, ilikuwa rahisi zaidi kufanya maamuzi ya kurejea Southampton. Ni fahari kubwa kuendelea kuwa sehemu ya kikosi hiki ambacho kilinipa malezi bora ya soka,” akasema Walcott kwa kuahidi kwamba atapania zaidi kuwa kielelezo kwa wanasoka chipukizi uwanjani St Mary’s.

Walcott aliwajbishwa katika kikosi cha watu wazima kambini mwa Southampton kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 2005 akiwa na umri wa miaka 16 na siku 143.

Hatua hiyo ilimfanya kuwa mchezaji wa umri mdogo zaidi kuwahi kuvalia jezi za kikosi cha kwanza cha Southampton.

Awali, Walcott alikuwa katika akademia ya Southampton na akawasaidia kutia kapuni ubingwa wa Kombe la FA kwa chipukizi mnamo 2005.

“Ipo historia ndefu ya mahusiano kati ya Walcott na Southampton,” akasema kocha wa Southampton, Ralph Hasenhuttl.

Uhamisho wa Walcott hadi Southampton ulichochewa na tukio la fowadi matata raia wa Argentina, Guido Carrillo, 29, kujiunga na kikosi cha Elche kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) bila ada yoyote.

Mbali na Carrillo, wanasoka wengine walioagana na Southampton ni fowadi raia wa Morocco, Sofiane Boufal, 27, aliyesajiliwa na Angers bila ada yoyote na Mholanzi Wesley Hoedt, 26, aliyerejea Lazio kwa mkopo wa mwaka mmoja. Southampton almaarufu ‘The Saints’, waliagana pia na kipa raia wa Uingereza, Angus Gunn, 24.