Habari

Walemavu 10 Thika wapata viti vyenye magurudumu

September 14th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WALEMAVU wapatao 10 kutoka eneo la Kilimambogo, Thika Mashariki wamenufaika kwa kupata viti vya kuwezesha mwendo vyenye magurudumu.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alifanya juhudi kuona ya kwamba walemavu hao wanapata viti hivyo.

Walemavu hao wanatoka vijiji vya Mukuneke na Maguguni eneo la Thika Mashariki.

Alisema baada ya uchunguzi kufanywa, ilibainika ya kwamba wengi wao wana familia na huwa vigumu kwao kujikimu kimaisha kwa sababu hawawezi kujitembeza wenyewe.

Mmoja wa walemavu akiwa kwenye kiti cha magurudumu. Picha/ Lawrence Ongaro

Mnamo Ijumaa, mbunge huyo alizuru maeneo hayo na kuwafaa.

“Nilipata ripoti kuwahusu walemavu hao na nikafanya juhudi kuona ya kwamba wanapata usaidizi haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Wainaina.

Alisema walemavu hao watapata bima ya kiafya ya NHIF kwa muda wa mwaka mmoja kwa lengo la kushughulikia afya yao.

Wakati huo pia walemavu hao watatengewa pahala spesheli katika soko kuu la Madaraka, Makongeni ili waweze kuuza bidhaa zao huko.

“Nitazungumza na wafanyabiashara wa soko hilo wakubali kuwakumbatia ili nao waweze kujitafutia riziki kama watu wengine. La muhimu pia ni kwamba, wateja wawe wakinunua bidhaa zao ili nao waweze kubarikiwa na Mungu,” alisema Bw Wainaina.

Akaongeza: “Nitafanya juhudi kuona ya kwamba kila mlemavu anapata mwavuli wa kujikinga jua wakati akifanya biashara.”

Mashinani

Afisa wa afya ya Jamii kwenye afisi ya CDF Thika, Bi Joyce Njeri alisema kuna walemavu wengi mashinani ambao wanatamani kupata usaidizi.

“Wengi wao wana shida ya viungo na kwa hivyo wakipata viti vya magurudumu watanufaika pakubwa,” alisema Bi Njeri, na kuongeza hata wengine huogopa kujitokeza ili “wajitambulishe kwetu kama wahudumu wao.”

Alisema kila mara wao huzuru maboma tofauti ili kuwatambua walemavu wanaotaka misaada ya vijigari aina hiyo.

Alizidi kueleza kuwa wengine bado wanawaficha wapendwa wao ambao ni walemavu.

Bi Mary Wambui ambaye ni mmoja wa walemavu hao aliyepokea viti hivyo, aliomba atafutiwe jambo la kufanya kama kufunguliwa biashara ili akidhi mahitaji ya familia yake.

“Mimi nina watoto wanaonitegemea na mara nyingi huwa ni vigumu kwangu kutoka nyumbani kwenda mbali kutafuta ajira,” alisema Bi Wambui, na kuongeza kuwa wamefurahia hatua ambayo mbunge wao alichukua ya kuwaletea usaidizi wa kudumu.

Bw Peter Gichina ni mwingine ambaye alinufaika pakubwa na msaada huo huku akipongeza hatua nzuri iliyochukuliwa na mbunge huyo.

“Sasa mimi natamani tu kuanzisha biashara ili niweze kujikimu kimaisha na familia yangu. Kama ninaweza kupata mahali penye kivuli ninaweza kujiendeleza kutokana na biashara,” alisema Bw Gichina.