Habari Mseto

Walemavu Gatundu Kaskazini wapata viti vya magurudumu

August 14th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WALEMAVU wanastahili kupata usaidizi wa dharura ikizingatiwa kwamba wanakabiliwa na masaibu na changamoto tele.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alisema imebainika kuwa mashinani, walemavu wameachwa pweke na ni vyema wapewe usaidizi wakati wowote.

Mbunge huyo alizuru kijiji cha Mitero eneo la Gatundu Kaskazini ambapo walemavu; wazee kwa watoto wapatao 30 walinufaika na viti vya magurudumu.

Alisema wengi wa walemavu hawapati haki katika jamii kwa sababu wengi wao hufichwa kwenye nyumba ili wasitambulike.

“Walemavu hawa waliopokea viti hivyo vya magurudumu watapata hafueni baada ya kubadilisha mwelekeo wa maisha yao,” alisema Bw Wainaina.

Alisema wakfu wa Jungle Foundation umejitolea kusaidia wasiojiweza kote nchini ambapo imekuwa ikibadilisha maisha ya jamii.

Alisikitika kwa kusema ya kwamba wakati huu wa Covid-19, walemavu wengi wamepitia maisha magumu kwa sababu wengi wao wanatambaa nchini huku kukiwa na matumaini mkubwa ya kugusa viini vya maambukizi sakafuni.

“Ninatoa mwito kwa wale walio na uwezo wa kifedha wawe mstari wa mbele kuona ya kwamba wanasaidia walemavu bila kuwabagua. Wengi hawana wa kumkimbilia kwa usaidizi,” alisema Bw Wainaina.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina (kulia). Picha/ Lawrence Ongaro

Wazazi walipewa changamoto kwa kuhimizwa kujitokeza na kukiri kuwa wana watoto walemavu badala ya kuwafungia nyumbani.

Alisema walemavu hao waliopokea magurudumu hayo wamepata hafueni kwa sababu watakuwa wakiendesha shughuli zao kwa urahisi bila kutegemea usaidizi wa kila mara.

Afisa anayesimamia afya ya jamii katika wakfu wa Jungle Foundation Bi Joyce Njeri, alisema kuna walemavu wengi mashinani ambao wanahitaji usaidizi wa dharura.

“Tayari tumezuru maeneo mengi hasa Thika Mashariki kama Kilimambogo, Muguga na Ndula ambako tumetoa viti vya magurudumu kwa walemavu wengi,” alisema Bi Njeri na kuongeza “natoa mwito kwa wazazi wenye walemavu wajitokeze ili wapate usaidizi.”

Bi Jane Wanjiku Njoroge, 68, ambaye ni mlemavu alishukuru wakfu wa Jungle kwa kuwajali walemavu.

“Mimi namshukuru kupata miguu spesheli ya kutembea, na kwa hivyo sitasumbua watu kila mara kwa kutembea nikitumia machela. Sasa nitajifanyia mambo yangu mengi mwenyewe,” alijitetea Bi Njoroge.

Aliiomba serikali kuhakikisha wakongwe wanapokea fedha zao za wazee bila kuchelewa kwa sababu hilo ndilo tegemeo lao.