Michezo

Walemavu Nakuru wanavyofurahia kucheza voliboli

February 24th, 2020 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Nakuru County Sitting Volleyball ni kikosi cha wachezaji wasiopungua 30 wanaocheza voliboli chini ya usimamizi wa mkufunzi Florence Ofwenje.

Kikosi hiki kimedhihirishia dunia kuwa mapungufu ya mwili sio kigezo cha kuonyesha uwezo wa mtu katika jukwaa lolote ilmuradi binadamu awe na bidii, hakuna kisichowezekana chini ya jua.

Wachezaji wengi hufika kila siku ya Jumanne na Alhamisi uwanjani Afraha kufanya mazoezi huku wengi wao wakiwa na mikongojo na viti vya magurudumu bila kujali makali ya jua na wakati mwingine mvua.

Ingawa wizara ya michezo ya kaunti haijaboresha mazingira ya kufanyia mazoezi ,inabidi wajikunyate chini ya kijumba kidogo kilichoezekwa paa tu bila madirisha wala mlango.

Motisha wanayopata kutoka kwa mkufunzi Florence Ofwenje imewapatia mtazamo tofauti katika maisha huku baadhi yao wakiamini kuwa kipaji kinaweza kumfikisha mtu mbali muradi ajiwekee malengo katika Maisha.

Wachezaji wa Nakuru County Sitting Volleyball wakifanya mazoezi uwanjani Afraha. Picha/ Richard Maosi

Kila mara wanaponyanyua mpira na kuupiziza kwenye nyavu zinazoning’inia, mashabiki hufurahia kuwatazama wengi wao wakiwamiminia sifa tele kwa kuinua jina la kaunti ya Nakuru ndani na nje ya nchi.

Mkufunzi Florence Ofwenje amejitolea kuhakikisha kuwa wachezaji hawa zaidi ya 30 hawakati tamaa maishani, licha ya serikali kutozingatia maslahi ya michezo miongoni mwa walemavu.

Anaona kuwa itakuwa ni jambo la afadhali endapo mchezo wa voliboli wa walemavu(sitting volley ball)utapata nafasi saw ana raga au kandanda ili kuimarisha ushindani baina ya wachezaji.

Anasema kuwa ni bora kubuniwa kwa ligi ya watu walemavu ambayo itashirikisha timu kutoka kwenye kaunti nyinginezo na kufuatilia mpangilio wa ratiba maalum.

Florence hulazimika kusafisha kwanza uwanja kabla ya wachezaji wake kuhudhuria mazoezi kila siku ya Jumanne na Alhamisi.“Harufu ya mkojo na takataka zinazotapakaa kila sehemu ni mojawapo ya changamoto kubwa inayochelewesha muda wa kufanya mazoezi,” akasema.

Aliongezea kuwa wengi wa wachezaji hap ani wafanyibiashara wenye kipato kidogo wanaojitegemea mjini Nakuru na hajui ni kwa nini wizara ya michezo haijatenga sehemu ya kipato yake kukidhi mahitaji ya walemavu.

Lakini hili halijazuia ari yake kuona kuwa wachezaji wanapata ufanisi na kujivunia tunu kutokana na jasho la bidii zao kila mara wanapoingia ugani kuchuana na timu hasimu.

Anasema kuwa kufanya mazoezi ni mojawapo ya mambo yanayompatia faraja maishani akiamini amekuwa kwenye mstari wa mbele, kuwasaidia walemavu kujitambua na kujipatia ujuzi wa maishani.

Florence anasema kuwa alianza kucheza voliboli akiwa kijana na sasa anarudisha mkono kwa jamii yake,kwa njia ya kipekee akilenga kuwafikia walemavu zaidi kutoka mashinani ambao mpaka sasa hawana mtu wa kuwashika mkono.

Licha ya kufanya kazi katika kampuni ya mawasiliano miaka ya mbeleni anaona kuwa itakuwa ni jambo,lenye tija endapo wachezaji walemavu hatimaye watafanikiwa katika juhudi za kufuata ndoto zao maishani.

“Wafahamu kuwa kujikubali na kujifunza ni baadhi ya mambo muhimu ambayo kila mchzaji anastahili kuzingatia endapo ana malengo ya kufanya vyema kwenye tasnia yake,”akasema.

Anakubali kuwa amejifunza mengi kutoka kwa wachezaji wake ambao wamejitolea kucheza voliboli na kuwa na mshikamano wa aina yake ambao hajawahi kushuhudia.

Wamekuwa wakifika uwanjani kwa wakati kufanya mazoezi, ni wepesi wa kuchangisha pesa za kushiriki michuano ya kirafiki nje ya kaunti ya Nakuru.

Licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi mkufunzi Flowrence Ofwenje anasema timu imefanikiwa kutoa wachezaji wanne kwa timu ya Taifa. Picha/Richard Maosi

Anasema kuwa timu imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi mojawapo ikiwa ni ukosefu wa jezi za kufanyia mazoezi na kushiriki mechi za kujipima nguvu, vilevile wamekuwa wakipata taabu kupata namna ya usafiri wanapopata mialiko ya michuano ya mbali.

Kwa upande mwingine nahodha Fred Omondi anasema sehemu ya kufanyia mazoezi haina hadhi ya uwanja wa kimataifa , hasa muda huu Nakuru inapolenga kujumuishwa miongoni mwa miji mikuu nchini.

“Hakuna vyoo , maji ya kunywa wala vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa kufanyamazoezi,”akasema.

Hata hivyo juhudi za Ofwenje zinaonekana kuzaa matunda kwa sababu wachezaji wake wanne hushiriki kwenye michuano ya ligi katika timu ya taifa nao ni Fred Omondi.James Mureithi, Purity Wangare naMargret Wanjiru.

Ofwenje anasema kuwa licha ya kufanya mazoezi na walemavu amekuwa akiwasaidia viziwi katika kikosikingine ambacho pia kinahitaji msaada wa kaunti ya Nakuru hususan wizara ya michezo.