Habari Mseto

Walemavu wanaounda sodo za kutumika tena waomba msaada

September 5th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

CHAMA kimoja cha kutetea haki za watu walemavu, katika kaunti ya Mombasa kinaiomba serikali kupiga jeki mradi wake wa kutengeneza sodo ambazo zinazoweza kutumika tena.

Akizungumza na Taifa Leo, mwanzilishi wa chama cha Tunaweza Women, Bi Charity Chahasi, alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa watoto wa kike wanapata bidhaa hizi za kudumisha usafi wakiwa katika hedhi.

Bi Chahasi alisema kuwa mradi wao umewapa matumaini wasichana wengi kwa kuwa kufikia sasa wamesambaza sodo hizo zaidi ya 8,000 katika kaunti tofauti humu nchini.

“Mradi huu umepokelewa vizuri na watu wengi. Tumesambaza sodo hizo zinazoweza kutumika tena katika kaunti za Mombasa, Tana River, Migori, Nairobi, Eldoret, Kilifi, Busia na Samburu,” akasema Bi Chahasi.

Alisema kuwa sodo hizo hazichafui mazingira zikilinganishwa na zile ambazo ziko sokoni.

Mwanzilishi wa chama cha kutetea haki za walemavu cha Tunaweza Women, Bi Charity Chahasi akishika mojawapo ya sodo zinazoweza kutumika tena. Chama hiki kinaomba msaada wa fedha kutoka kwa serikali ili waweze kutengeneza bidhaa hiyo kwa wingi. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Sodo hizi pia zinahakikisha kuwa mazingira hayachafuliwi na bei yake ni nafuu. Tumezitumia na wasichana pia wanaweza kuzitumia,” akasema.

Naibu mwanzilishi wa chama hicho, Bi Lucy Chesi Naibu naye aliliomba Baraza la Kitaifa la Watu wenye Ulemavu Nchini (NCPWD) kuwaelezea ni vipi pesa za COVID-19 za walemavu zilitumika.

Bi Chesi alilikosoa baraza hilo kwa kukaa kimya kuhusu fedha zilizotengewa walemavu wakati huu wa janga la corona.

“NCPWD ni shirika la kiserikali na inapaswa kutuelezea kiasi gani cha fedha kilitengwa kwa ajili ya walemavu kote nchini,” akasema Bi Chesi.

Pia, Bi Chesi aliiomba serikali isiwatenge vijana walemavu katika miradi kama vile mradi wa kudumisha usafi nchini maarufu kama Kazi Mtaani.

“Kuna vijana wengu wenye ulemavu, pia hao wajumuishwe katika miradi hii,” akasema.