Habari Mseto

Walemavu wapokea viti vya magurudumu Kiambu

September 24th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

BAADA ya malalamishi kuhusu walemavu kunyimwa viti vya magurudumu kusambaa, sasa wamepokea viti hivyo jana Jumatano.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alizuru Ndumberi na Githunguri, na kutoa viti vya magurudumu 300 kwa walemavu hao.

Huku walemavu wakipokea viti hivyo pia wakfu wa Jungle Foundation ulipeana chakula kwa walemavu huku vifaa hivyo vikigharimu Sh 4 milioni.

” Azma yangu ya kupeana misaada kwa walemavu haiwezi sitishwa na yeyote na kwa hivyo nimelazimka kufika hapa na kupeana viti hivi vya magurudumu,” alisema Bw Wainaina.

Bw Michael Njoroge ambaye ni mnufaika amepongeza hatua hiyo akisema kilio cha haki kimetimia.

“Sisi walemavu Mungu aliye juu amesikia kilio chetu na kwa hivyo leo tumeona mkono wake,” amesema Bw Njoroge.

Amesema maisha yake yamebadilika pakubwa kwa sababu sasa atajitegemea kwa mambo yake.

Naye Simon Ngugi kutoka mji wa Thika, ambaye pia ni mlemavu,alitaja hatua hiyo kama maajabu ya Mungu.

“Baada ya kukosa viti hivi siku chache zilizopita sasa mwangaza umeonekana na tumepata msaada huo,” alisema Bw Ngugi.

Ilidaiwa kuwa wapinzani wa mbunge huyo wa siasa ndio walikuwa mstari wa mbele kuzima mpango huo.

Hata hivyo siasa za mwaka wa 2022 zimeshika kasi huku ikidaiwa mbunge wa Thika analenga kuwania kiti cha juu; cha ugavana.

Hiyo sio mara ya kwanza mbunge huyo kupitia masaibu mengi. Miradi mingi anayoanzisha imekuwa ikizimwa kwa kile kinatajwa kama kuvuka mipaka katika sehemu zisizo zake.

“Ninajua ya kwamba wananchi sasa wameelewa viongozi wanaoweza kujali maslahi yao, na kwa hivyo wasijaribu kucheza na maisha yao,” alisema mbunge huyo.

Wakati wa hafla hiyo wakazi wa maeneo hayo walifurika huko kujionea jinsi walemavu walivyopokea viti vyao, huku walemavu hao wakirejea nyumbani na kiti chake cha magurudumu.