Makala

WALENISI: Usawiri wa athari za ujinga na mifumo ya kibepari

April 19th, 2018 2 min read

Mwandishi: Katama Mkangi
Mchapishaji: East African Educational Publishers
Mhakiki: Wanderi Kamau
Kitabu: Riwaya
Jina la Utungo: Walenisi
Kurasa: 217

Na WANDERI KAMAU

MAREHEMU Katama Mkangi alikuwa miongoni mwa wasomi wachache wa Kiswahili ambao waliamini na kushadidia nadharia ya usoshalisti (ujamaa) kama nguzo kuu ya jamii endelevu.

Kwa namna moja, itikadi zake za kinadharia ndizo zilionekana kumsukuma pakubwa kwa vitendo vyake; uandishi na imani za kisiasa.

Msukumo huo ndio ulimpelekea kuandika riwaya ‘Walenisi’, ambayo ni usawiri wa athari za ujinga na mfumo kandamizi wa kibepari katika jamii yoyote ile.

Aidha, anawasilisha ujumbe huo kupitia Dzombo-aliye mhusika mkuu katika riwaya hii ya kijazanda.

Kwanza, uozo wa mfumo wa utoaji haki unajitokeza mwanzoni mwa riwaya hii, ambapo Dzombo anafikishwa mahakamani kwa makosa ambayo hakuwa ameyafanya.

Kitaswira, mahakama hiyo iko Duniani. Anakejeliwa na umati uliokuwa umefika. Anapewa adhabu ya kifo.

Adhabu hiyo ilitarajiwa kutolewa na chombo, kiitwacho sayari, ambacho kingemsafirisha kusikojulikana na hatimaye kumuua.

Isitoshe, madhumuni ya kuundwa kwa chombo hicho yamebadilishwa. Badala ya kutumiwa kufanyia utafiti kwa minajili ya kuimarisha maisha yao, kinatumiwa kuwakandamiza.

Licha ya hayo, kuna wale waliomwona kama mtetezi na sauti yao. Kimsingi, kudhalilishwa kwa Dzombo na mfumo kandamizi wa haki kunazua taswira ya mtaasisiko wa asasi za kisheria katika nchi za Afrika na jamii ya sasa.

Kingine kuu kinachojitokeza riwayani ni ‘majabali’ yanayoiandama jamii. Mwandishi anatumia jazanda ya Jabali la Ujinga kuashiria athari za ukosefu wa elimu na mzinduko wa kimawazo katika jamii. Hayo ndiyo yanapelekea kunyanyaswa kwake, hata anapopanda chakula cha kujitegemea na serikali.

Riwaya hii pia inazamia manufaa halisi ya mfumo wa ujima katika jamii, kufuatia makaribisho mazuri ambayo Dzombo anapokea kutoka kwa familia ya Mzee Mtu Maanani.

Mfumo wa kimaisha katika familia hii ni wa kujaliana, kinyume na hali ilivyo Duniani, kwani wale ambao walitetea haki na ukweli walihukumiwa kifo (kama alivyofanywa).

Matukio hayo yote yanamfanya Dzombo kuzamia utafiti wa kina, anaofanya kuhusu asili ya jamii ya Wachuna (wanaokisiwa kuwa waanzilishi wa mfumo wa kibepari).

Urejeleo wa asili yao ni: “Walizuka katika jamii na kuwanyima wenzao mahitaji ya kimsingi.” Ni katika enzi yao ambapo hali ya ufukara ilikita katika jamii.

Hata hivyo, kuna mapambazuko mapya ya uwepo wa utawala wa Wawalenisi, wanaoshadidia mfumo wa ujamaa kama njia kuu ya kuleta usawa katika jamii.

Baadhi ya vigezo vya kuleta umoja miongoni mwao ni utaifishaji wa viwanda kwa manufaa ya kila mtu.

Bila shaka, riwaya hii ni ukemeo mkuu kwa mfumo wa kibepari, ambao umekumbatiwa na jamii nyingi za kisasa.

Baruapepe: [email protected]