Wales wateremshwa ngazi kwenye Nations League baada ya kutandikwa na Poland

Wales wateremshwa ngazi kwenye Nations League baada ya kutandikwa na Poland

Na MASHIRIKA

WALES waliteremshwa ngazi kutoka makundi ya vikosi vya haiba kubwa kwenye Uefa Nations League baada ya Poland kuwapepeta 1-0 mnamo Jumapili usiku jijini Cardiff.

Poland waliohitaji sare ya aina yoyote dhidi ya Wales ili kukwepa shoka la kuwashusha daraja, walitamalaki mchezo katika kipindi cha kwanza ila wakakosa kufunga bao.

Iliwalazimu kusubiri hadi dakika ya 57 kufungiwa bao na Karol Swiderski aliyemegewa krosi na Robert Lewandowski ambaye pia alimtatiza pakubwa kipa Wayne Hennessey.

Japo Wales walikuwa na fursa nyingi za kusawazisha, walizipoteza nafasi hizo kupitia kwa Brennan Johnson na Gareth Bale walioshindwa kumzidi ujanja kipa Wojciech Szczesny.

Matokeo hayo yalisaza Wales wakivuta mkia katika Kundi A4 kwa alama moja pekee kutokana na mechi sita katika kampeni zao za kwanza kabisa kwenye Nations League.

Chini ya kocha Robert Page, mchuano ujao wa Wales ni gozi la Kombe la Dunia watakaloshiriki kwa mara ya kwanza baada ya miaka 64. Watafungua kipute hicho kitakachofanyika nchini Qatar kati ya Novemba na Disemba 2022 dhidi ya Amerika mnamo Novemba 21, 2022.

Page amekiri kuwa kuzamishwa kwao na Poland kulichangiwa zaidi na kutokuwepo kwa masogora Aaron Ramsey, Joe Allen, Harry Wilson na Ben Davies wanaouguza majeraha. Ethan Ampadu na Chris Mepham nao wanauguza majeraha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Gachagua aibuka bingwa wa kuteleza

Uholanzi, Croatia zatinga 4-bora

T L