Habari za Kaunti

Walevi Kirinyaga wafurika Nyeri baa zao zikifungwa

February 22nd, 2024 2 min read

NA STEPHEN MUNYIRI

WALEVI wanatoka Kaunti Kirinyaga wameanza kufurika katika baa na vilabu mjini Karatina, Kaunti ya Nyeri kukata kiu yao baada ya serikali inayoongozwa na Gavana Anne Waiguru kuamuru baa zote kufungwa kutokana na vifo vya watu 17.

Mji wa Karatina uko karibu na mpaka wa Kaunti za Nyeri na Kirinyaga. Maeneo ya burudani ya Nyeri yameripoti kuwa idadi ya wateja kutoka Kirinyaga inaendelea kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

Kinachoshangaza ni kwamba walevi kutoka Kirinyaga wamepata mahali salama pa kukata kiu Karatina ambako ni makao makuu ya eneo bunge la Mathira, nyumbani kwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye kwa sasa anaongoza kampeni kubwa ya kuangamiza ulevi eneo la Kati ya Kenya.

Wahudumu wengi wa baa waliozungumza na Taifa Leo walisema kwamba kuna wimbi jipya la wanywaji tangu kufungwa kwa baa za Kirinyaga.

“Japo tunawahurumia wenzetu wa Kirinyaga kwa masaibu yao, sisi pia hatulalamiki, kwani tunafanya biashara nzuri, mauzo yetu ya kila siku yameongezeka sana tangu Gavana Waiguru alipoamuru kufungwa kwa baa za Kirinyaga.

“Tunafanya biashara nzuri, Jumatano nilikuwa na angalau wateja 16 wapya kutoka Kirinyaga,” akasema Bw Francis Maina, meneja katika baa ya Quality.

“Wakazi wa Kirinyaga wanaovuka mpaka kupata burudani hapa wameongezeka, tunaweza kutambua wateja wetu wapya kutoka Kirinyaga kwa urahisi kwa sababu ya lafudhi yao nzito ya Ndia na Gichugu na wanamlaumu gavana wao kwa masaibu yao na wanatuambia wanatumai atarejesha biashara ya vileo Kirinyaga katika hali ya kawaida” alisema mmiliki mwingine wa baa katika kituo cha kibiashara cha Kiaruhiu.

Kufungwa kwa baa na vilabu vya pombe katika Kaunti ya Kirinyaga hakukufurahisha baadhi ya wahudumu wa baa na wakazi ambao wamepinga hatua hiyo.

“Hii si haki kwetu. Kufunga vilabu vya pombe hakumaanishi kuwa kila mtu atakuwa askofu ghafla, ni haki yetu kufurahia kinywaji tunachochagua,” aliteta Joseph Murimi, mkazi wa Kerugoya mjini.

Alilalamika kuwa watu wanaopenda pombe wanakabiliwa na wakati mgumu kwa sababu hawana pa kupata kileo katika Kaunti ya Kirinyaga.