Habari Mseto

Walevi kutoka Nyeri wafurika Kirinyaga kukata kiu

April 1st, 2024 1 min read

NA STEPHEN MUNYIRI

MAMIA ya waraibu wa pombe katika eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri, sasa wamekimbilia Kaunti ya Kirinyaga baada ya baa karibu 400 kufungwa mjini Nyeri kufuatia kampeni kali inayoongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Katika mkondo tofauti, waraibu wa pombe mjini Mathira waliowapokea wenzao kutoka Kirinyaga baada ya Gavana Waiguru kufunga vituo vya pombe, sasa wamefurika katika maeneo ya Kiangai, Kagumo na mji wa Kerugoya.

Mnamo Februari 2024, mji wa Karatina ulishuhudia waraibu wa pombe wakivuka kukata kiu eneo hilo baada ya Kaunti ya Kirinyaga kuagiza baa zote zifungwe kufuatia vifo vya watu 17.

Udadisi uliofanywa na Taifa Dijitali tangu Ijumaa, umeonyesha wapenda burudani walikuwa na Sikukuu kavu zaidi ya Pasaka ikilinganishwa na miaka iliyotangulia ambapo watu wangeonekana wakifurahia vinywaji na nyama choma, huku vilabu vikifungwa.

Hali imegeuka kuwa kama wakati wa janga la Covid-19 ambapo hakukuwa na ishara ya muziki uliosikika kutoka vituo vya pombe wala walevi walioonekana wakiyumbayumba kuelekea makwao.

Wafanyabiashara viungani mwa Kirinyaga waliozungumza na Taifa Dijitali walisema wameshuhudia ongezeko la wateja tangu baa zilipofungwa Mathira.

“Tunahurumia wenzetu eneo la Mathira kwa sababu tulipitia hali kama hiyo Februari, mabadiliko haya yanatukumbusha kuwa maisha hugeuka na tunapaswa kila mara kupokea fursa na uwezekano mpya,” alisema mmiliki wa baa kwa jina Naftali Njogu.