Habari

Walibora alitabiri kifo chake

April 21st, 2020 5 min read

NA MARY WANGARI

[email protected]

Huku taifa na ulimwengu kwa jumla ukiwa umetikiswa na habari za kutisha kuhusu kifo cha mwandishi nguli Profesa Ken Walibora, imebainika kwamba marehemu huenda alitabiri kuhusu kifo chake miaka mingi iliyopita katika vitabu alivyoandika.

Haya yanajiri wakati ambapo kifo cha kutatanisha cha msomi huyo kimesalia kitendawili kigumu hasa kufuatia ripoti ya upasuaji iliyotolewa na mwanapatholojia mkuu Johansen Oduor.

Profesa Walibora alikuwa mwandishi aliyebobea aliyekuwa na ustadi wa kusawiri matukio katika jamii kwa usanifu mkubwa kwa ufasaha kupitia lugha ya Kiswahili.

Utabiri katika vitabu vyake vya fasihi ulitimia kwa usahihi wa kiwango cha juu kiasi kwamba baadhi ya wachanganuzi walimwona kama nabii.

Hata hivyo, hakuna aliyetarajia kwamba mwanafasihi huyo tajika, angetabiri kuhusu kifo chake kwa njia bayana jinsi alivyofanya katika vitabu vyake alivyoandika zaidi ya miaka 10 iliyopita: Siku Njema (1996) na Kidagaa Kimemwozea (2012).

Uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi andishi za gwiji huyo, zinadhihirisha ulinganifu unaolandana kwa kiasi kikubwa na matukio kabla ya kifo chake.

Kuanzia kutoweka kwake kwa siku kadhaa kabla ya kupatikana akiwa amefariki, mazingira ya kutatanisha ambapo alikumbana na kifo chake, kutelekezwa na madaktari na wauguzi na baadaye kufariki hospitalini hadi namna ya mazishi yake yalivyofanyika.

Kulingana na msuko wa matukio yote hayo, ni kana kwamba marehemu Walibora alikuwa na maono kuhusu jinsi atakavyoaga buriani jukwaa la ulimwengu huu.

Iwe ni mkosi, bahati mbaya au sadfa tu iliyojitokeza katika sanaa ya uandishi wake wa fasihi, ni kwako wewe msomaji kuamua, kupitia uchambuzi na ulinganifu huu wa mwandishi huyo na wahusika aliowabuni.

Kulingana na ripoti za polisi, marehemu Walibora alitoweka ghafla mnamo Ijumaa, Aprili 6. 2020, huku jamaa na familia yake wakiijitahidi kumsaka kila mahali kwa muda wa siku nne bila kufua dafu.

Vivyo hivyo, katika riwaya aliyhoandika Walibora ya Kidagaa Kimemwozea, mhusika Nasaba Bora Mtemi wa eneo la Sokomoko, anatoweka kwa siku kadhaa huku familia yake ikiachwa kumtafuta kila pembe bila kujua alipo.

“Uliibuka uvumi kwamba Mtemi Nasaba Bora amepotea, hajulikani alipo. Kenda arijojo kama tiara ipeperushwayo na kimbunga. Alisakwa kila mahali asipatikane…” (ukurasa 152).

Mwili wa mwendazake Walibora uliripotiwa kupatikana na jamaa zake siku nne baadaye mnamo Jumatano, Aprili 10, 2020, katika mochari ya Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) tangu alipotoweka kwa njia ya kutatanisha.

Kwa njia sawia, baada ya kumsaka kwa siku kadhaa, familia ya Mtemi Nasaba Bora inaupata mwili wake ukining’inia kwenye mti wa mkuyu msituni akiwa tayari ameaga dunia baada ya kujitia kitanzi (ukurasa 159).

Hatima ya mwandishi Walibora na mhusika Mtemi Nasaba inafanana pakubwa tofauti ikiwa huku mwili wa mhusika wake ukipatikana msituni baada ya kujitia kitanzi, mwili wa Walibora, ulipatikana kwenye mochari baada ya ajali.

Funguo za gari na stakabadhi za vitambulisho vya mwandishi huyo vilikabidhiwa polisi na vijana wa mitaani baada ya marehemu kuripotiwa kugongwa na matatu almaarufu Double M katika Barabara ya Landhies

Hata hivyo, gari lake aina ya Mercedes Benz lilipatikana likiwa limeegeshwa katika eneo la Kijabe Street umbali wa takriban kilomita tatu kutoka mahali ambapo mwandishi huyo alidaiwa kukumbana na ajali.

Mkuu wa Polisi katika Kituo cha Central Mark Wanjala alieleza kwamba walipokea habari kutoka kwa mlinzi wa duka mojawapo kwamba gari hilo lilikuwa limekaa hapo kwa muda wa siku nne na lilikuwa likifungia maduka.

Hii ni ithbati tosha kwamba marehemu aliegesha gari lake sehemu hiyo kabla ya kuondoka kwa miguu na kuelekea kokote alipokuwa ameenda kabla ya kukumbana na kifo chake cha kutatanisha.

Vivyo hivyo, gari la mhusika Mtemi Nasaba Bora linapatikana likiwa limeegeshwa katika eneo tofauti na ambapo mwili wake unapatikana msituni.

“Ila gari lake ndilo lililobaki limeegeshwa karibu na jumba la Majinuni. Ilikuwa dhahiri kwamba alipoondoka hakuondoka kwa gari hilo…” (uku 159)

Sawa na jinsi Walibora alivyofariki baada ya kugongwa na gari, katika riwaya yake tajika ya Siku Njema, mhusika Rashid pia anafariki baada ya kuhusika katika ajali. (Ukurasa 11).

Ni baada tu ya mwili wa Rashid kupatikana, ndipo polisi wanapoanzisha uchunguzi kubaini kiini cha kifo chake. Hii inawiana na jinsi hali ilivyo kuhusu kifo cha Walibora.

Rashid alifariki katika ajali ya gari akiwa njiani kutoka Mombasa kwenda Lamu siku tatu tu kabla ya harusi yake na Zawadi.

“Hata hivyo, rashid hakujaliwa kufika Lamu kwani basi hilo lilipata ajali karibu na kituo cha polisi cha Bamburi na hapo akafariki

Katika Kidagaa Kimemwozea, mwandishi anatueleza jinsi mhusika Uhuru ambaye ni mtoto, anafariki baada ya kukosa huduma za matibabu kutokana na utepetevu wa wauguzi katika Zahanati ya Nasaba Bora.

Imani na Amani walitoka na Uhuru na kumpekleka katika zahanati ya Nasaba Bora. Walipofika si mabezo hayo waliyofanyiwa na wauguzi wa kike waliokuwa wanafuma fulana zao na kupiga zohali (uku 76)

“Amani akakitwaa kitoto mikononi mwa Amani ili kumisaidia kukibeba. Kikakohoa punde. Lilikuwa kohozi kavu. Kilikuwa kimenyongea na kunyong’onyea mno, hakina udole kitoto hicho. Kikaanza kufafaruka mikononi mwa Amani na kupumua kwa shida kama mgonjwa wa pumu. Kikanyosha miguu na mikono na kutulia tuli. Kikawa baridi kama barafu.” (uk 77)

Sawia na mhusika Uhuru, ripoti zinaashiria kwamba, Walibora vilevile alikata kamba katika kitengo cha dharura KNH baada ya kusubiri huku akivuja damu kwa saa 18, bila kuhudumiwa na matabibu, tangu alipokimbizwa hospitalini humo saa nne asubuhi hadi alipofariki saa sita usiku wa manane.

Hivyo basi kiini cha kifo cha mwandishi yamkini kilitokana na kutelekezwa na wahudumu wa afya katika hospitali hiyo ya umma sawasawa na yaliyomkumba mhusika wake Uhuru.

Aidha, katika Kidagaa Kimemwozea, mhusika DJ Bob anakimbilia hospitali ya Nasaba Bora ili kupata msaada wa kimatibabu baada ya kung’atwa na mbwa anayeugua maradhi hatari ya kichaa cha mbwa (uk 98).

Hata hivyo, baada ya kukaa hospitalini humo kwa muda pasipo dalili ya kupata matibabu yoyote, analazimika kumwendea rafiki yake ambaye alimtibu kwa kutumia mitishamba hadi alipopata afueni.

Laiti mwandishi Walibora angelikuwa na uwezo wa kuondoka KNH na kutafuta matibabu kwingineko! Huenda angelinusurika mauti sawia na mhusika wake DJ Bob. Lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo na akafariki akisubiri kuhudumiwa.

Isitoshe, katika riwaya ya Siku Njema, mwili wa mhusika Juma Mkosi au Mzee Kazikwisha unapatikana na mwanawe Msanifu Kombo, siku kadhaa baada ya kifo chake sawia na jinsi mwili wa Walibora ulivyopatikana siku nne baadaye tangu alipokumbana na mauti.

Aidha, mwili wa mhusika huyo ulipopatikana, wengi hawakufahamu alikuwa ni Juma Mkosi msomi wa kutajika.

“Mwili wa Mzee Kazikwisha ulipatikana na mwanawe Msanifu Kombo Siku Kadha baada ya kifo chake. Hakujulikana na wengi kuwa alikuwa Juma Mukosi, msomi wa kutajika.” (uk 134)

Vivyo hivyo, licha ya umaarufu na sifa zake za uandishi wa fasihi kutamba nchini na kimataifa, mwili wa msomi huyo ulipopatikana hatimaye, wengi hawakuweza kumtambua ikiwemo jamaa zake.

Inadaiwa kuwa ililazimu mamake kuitwa ili kumtambulisha.

Hatimaye, katika Kidagaa Kimemwozea, licha ya mhusika Nasaba Bora kuwa na hadhi ya mtemi ambayo ni sawa na mfalme, katika eneo la Sokomoko, mazishi yake yalihudhuriwa na watu 10 pekee kinyume na ilivyotarajiwa kwa mazishi ya kiongozi wa cheo kama hicho.

“Waombolezaji walikuwa wa kuhesabu wakiwemo…,” (uk 159)

Mhusika Juma Mkosi au Mzee Kazi Kwisha, licha ya sifa zake kama msomi tajika, anazikwa katika mazishi yaliyohudhuriwa na watu wachache tu, katika Siku Njema.

“Maziko ya Juma Mukosi yalihudhuriwa na idadi ndogo sana ya watu.”(uk 135)

Inasikitisha mno kwamba sawia na mazishi yake wahusika wake Mzee Kazi Kwisha na Mtemi Nasaba Bora, mazishi ya mwandishi nguli Walibora yanatarajiwa kuhudhuriwa na watu wachache tu wasiozidi 15, hasa jamaa na familia yake, licha ya umaarufu wake katika tasnia ya fasihi andishi.

Maelfu ya marafiki, wasomi, mashabiki na magwiji mbalimbali aliotagusana nao wakati wa uhai wake, hawatapata fursa ya kumuaga buriani na kumpa heshima stahiki ya mwisho, ikizingatiwa kuwa kifo chake kimejiri wakati wa janga la Covid-19, ambalo limeyumbisha taifa na ulimwengu wote.