Makala

WALIBORA: Uvumbuzi wa Kiafrika kwa matatizo yao ni hatua kubwa

November 24th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA

Kudidimia kwa utashi wa bidhaa za Afrika nchini Marekani, Ulaya na kwingineko kumechochea ari ya nchi za Kiafrika kufanya biashara zenyewe kwa zenyewe.

Tokeo la ari hii ni kuundwa kwa Mwafaka wa Soko Huria Barani, yaani African Continental Free Trade Area (AfCFTA). Kwa kweli bara hili litapata hasara kubwa sana endapo litaendelea kutegemea masoko ya nje ya mipaka yake ili kuwa na maendeleo endelevu.

Yamkini sasa Afrika imebaini kwamba ipo haja ya kuchukua hatua mwafaka kulipatia ufumbuzi suala hili, ufumbuzi wa Kiafrika kwa matatizo ya Afrika.

Jiji kuu la Ethiopia, Addis Ababa mnamo Novemba 26 hadi 27, 2019 litakuwa mwenyewe wa mazungumzo kuhusu utekelezaji wa Muafaka wa Soko Huru Afrika. Kongomano hilo litawajumuisha wadau toka asasi za serikali na zisizo za serikali pamoja na wafanyabiashara kote barani kujadili utekelezaji.

Wajumbe hao 70 watapata fursa nzuri ya kuelewa na kupanga mikakati ya utekelezaji wa muafaka huo wa kurahisisha biashara baina ya mataifa ya Kiafrika kwa kuondoa vikwazo zisivyokuwa na tija.

Mataifa ya Afrika yameng’amua kwamba wale waitwao washirika wa kimaendeleo kutoka mataifa yaliyoendelea, huenda hawatataka hasa kwa dhati Afrika iendelee bali ibakie nyuma siku zote.

Ni dhahiri kwamba kwa sasa mataifa haya ya Kiafrika yameazimia kujikwamua yenyewe kwa kufanya biashara yenyewe kwa yenyewe ili kuepuka kurubuniwa na wanafiki wa dunia.

Kubuniwa kwa Muafaka wa Soko Huru Afrika mnamo Mei, 2019 ni matokeo ya juhudi za pamoja za miongo mingi zenye lengo la kutangamanisha biashara kote barani Afrika ili kuliwezesha kushindana vilivyo na mabara mengine.

Ni muhimu kutambua hamasa ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM) kushiriki katika biashara ya wao kwa wao.

Taarifa ya sekretariati ya JAM ya 2018 inataja kwamba biashara baina ya nchi za Afrika Mashariki iliongezeka hadi Sh5.98 bilioni mwaka 2018 toka Sh5.46 bilioni mwaka uliotangulia wa 2017.

Isitoshe, tukio la kihistoria la kutia saini mkataba wa AfCFTA lililotekelezwa na mataifa 44 kutoka jumla ya 55 barani Afrika, lilitokea kwenye jiji la Kigali, Rwanda katika eneo la Afrika Mashariki.

Aidha, mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya ikiwemo, yalikuwa miongoni mwa yale ya kwanza kabisa kuidhinisha muafaka huo.

Hapana shaka kubuniwa kwa Muafaka wa Soko Huru Barani Afrika kunaendena na mawanio ya waasisi wa mataifa ya Afrika kama vile Kenneth Kaunda, Kwame Nkrumah, Jomo Kenyatta na Julius Kambarage Nyerere.

Afrika haiwezi kuendelea kuwa mtegemezi wa washirika wanafiki katika harakati zake za biashara. Inapaswa kupanga mikakati ya kujitegemea kwa kufanya biashara ndani na baina ya mataifa yake kuwa rahisi.

Vinginevyo, Afrika itajikuta inadidimia tena katika lindi la ukoloni mpya huku iking’ang’aniwa tena kama mpira wa kona kutokana na rasilmali zake!