Dondoo

Walimania zamu ya kualika vipusa

July 14th, 2019 1 min read

NA JOHN MUSYOKI

KIEMBENI, MOMBASA

KULISHUHUDIWA sinema ya bure mtaani hapa makalameni walipotwangana wakizozania zamu ya kujivinjari na kipusa chumbani. Duru za mtaani zinasema wawili hao walikuwa wamekodi chumba cha kulala kwenye ploti na mzozo ulizuka walipoanza kunyemelea vipusa mtaani.

Juzi jamaa mmoja alisikika akimlaumu mwenzake kwa kumharibia mipango yake alipomwalika kipusa chumbani bila kumuarifu.

“Wewe ni mtu kisirani sana. Kwa nini ulimemleta mpenzi wako hapa chumbani na haukuwa umeniarifu. Juzi uliburudika na mpenzi wako hapa chumbani. Leo ilikuwa zamu yangu na mpenzi wangu yuko njiani anakuja,” jamaa alimlaumu mwenzake.

Hata hivyo, jamaa alishikilia kuwa mpenzi wake hangeondoka. “Itabidi uahirishe miadi yako na mtu wako hadi kesho ama siku nyingine,” jamaa alifoka.

Inasemekana wawili hao walirukiana na kuanza kutwangana magumi na mateke. “Toka nje na kahaba wako. Leo ni siku yangu na sitakubali unikatizie starehe zangu,” polo alimwambia mwenzake huku akimlisha kichapo.

Inaarifiwa kuwa wapangaji walivutiwa na kioja hicho na kwenda kutazama sinema ya bure. Baadhi ya wapangaji hao waliingilia kati na kuwatenganisha wawili hao. Kipusa alipoona vurumani zikizidi, alitoka shoti kuhepa zogo hilo.

Kulingana na mdokezi, ilibidi landilodi kuitwa kutuliza hali. Baada ya kupashwa kilichotokea aliamua kuwafurusha wawili hao.

“Nyinyi vijana, tabia yenu imenifika shingoni. Kesho, ondokeni katika ploti yangu. Hamtageuza ploti yangu kuwa lojingi,” landilodi alisikika akiwaambia mapolo hao.

Inasemekana amani ilirejea plotini baada ya wawili hao kufukuzwa. Kioja cha wanaume hao kilibaki kuwa gumzo mtaani.