Habari

Walimu wa chekechea Nairobi waibua madai mazito

February 20th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

CHAMA cha Walimu wa Chekechea katika Kaunti ya Nairobi kinamtaka Gavana Mike Sonko kuwachukulia hatua baadhi ya maafisa wakuu wa serikali yake, kikiwashutumu kuwaitisha hongo ya Sh150,000 ili kuwaajiri.

Walimu hao wamekuwa wakifunza kwa kujitolea ila kuna nafasi kadhaa za kazi ambazo zimetangazwa na serikali hiyo.

Kulingana na mwenyekiti wa walimu hao, Lawrence Otunga, juhudi zao kushinikiza uwazi katika mchakato wa ajira hizo zimekuwa zikiingiliwa na baadhi ya maafisa wakuu wa kaunti.

“Hapa baadhi ya maafisa wanaingilia shughuli na mchakato wa ajira,” amesema Bw Otunga.

Bw Lawrence Otunga akiwahutubia wanahabari katika eneo la Freedom Corner. Picha / Wanderi Kamau

 

Hii ni licha ya wengi wao kujitolea kufunza bila malipo kwa muda mrefu.

“Wanachama wetu karibu kumi wameambiwa kutoa hongo ikiwa wanataka kuajiriwa. Hii ni licha yao kujitolea kwa kuda mrefu kufunza katika shule za chekechea bila mishahara kwa muda mrefu,” akasema Bw Otunga.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba walimu hao wanapaswa kupewa kipao mbele katika nafasi hizo, ikizingatiwa kwamba wengi wao wametimiza viwango vilivyowekwa na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC).

“Tunamwomba gavana wetu kuhakikisha kwamba wanachama wetu wamezingatiwa katika nafasi hizo. Ni kinaya kwamba wanatishwa na kuitishwa hongo, baada ya kupewa ajira hizo kama shukrani kwa huduma ambazo wamekuwa wakitoa kwa kaunti,” akasema mwenyekiti huyo.

Walimu hao walifanya maandamano ya amani kutoka eneo la Freedom Corner, Nairobi hadi katika Ukumbi wa City Hall kuwasilisha malalamishi yao, ila hakuna aliyekuwepo kuyapokea.

Gavana Sonko amekuwa akisisitiza kwamba masuala yote ya uajiri katika kaunti yake yamekuwa yakiendeshwa kwa njia ya uwazi.

Mwezi uliopita, aliyekuwa Waziri wa Elimu katika kaunti hiyo Janet Ouko alijiuzulu akilalamikia kuingiliwa kwa utendakazi wake na Bw Sonko.

Gavana huyo alimteua Bi Lucia Mulwa kuchukua nafasi yake.