Habari

Walimu waitaka serikali kuu kutwaa usimamizi wa elimu ya chekechea

August 14th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

WALIMU wa shule za chekechea walisema Jumatano kwamba wanataka usimamizi wa elimu ya nasari kurejeshewa serikali ya kitaifa badala ya serikali za kaunti, wakilalamika zimeshindwa kuisimamia ifaavyo.

Walimu hao walisema kuwa serikali nyingi za kaunti zimekuwa zikipuuzilia mbali masuala muhimu kama ulipaji mishahara yao na uwekezaji katika miundomsingi muhimu.

Kupitia Chama cha Walimu wa Chekechea Kenya (Teyeta), walisema kuwa hilo ni mojawapo ya masuala makuu wanayotaka yashughulikiwe na Jopo la Maridhiano (BBI) linalpoandaa ripoti yake kuhusu mageuzi ya Katiba.

“Elimu ya nasari imedorora nchini tangu ilipoanza kusimamiwa na serikali za kaunti. Zimeiharibu kabisa. Kwa mfano, utaratibu wa kuwaajiri watu hauzingatii viwango vyao vya masomo walivyo navyo, mbali vile wanavyofahamiana na wasimamizi wake wakuu. Ni hali ambayo pia imewanyima nafasi walimu ambao wamehitimu vizuri,” akasema Bw Lawrence Otunga, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho.

Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Walimu wa Chekechea Kenya (Teyeta) Bw Lawrence Otunga akihutubu Agosti 14, 2019, jijini Nairobi. Picha/ Wanderi Kamau

Wakiwahutubia wanahabari jijini Nairobi, walimu hao walilalama kwamba wamekuwa wakilipwa mishahara duni ya kati ya Sh3,000 na Sh10,000 licha yao kuzishinikiza serikali husika kuitathmini upya kutokana na changamoto ambazo huwa wanakumbana nazo.

Walisema kuwa kando na kulipwa mishahara hiyo, wengi wao wamekuwa wakicheleweshwa kulipwa, wakati mwingine wakitumiwa mishahara nusu kwa njia ya M-Pesa.

“Tunapitia changamoto nyingi za kifedha licha ya wanachama wengi wetu kuwa wamesoma na kuhitimu katika viwango mbalimbali vya elimu. Licha ya juhudi hizo zote, ni kama kwamba hawatambuliki na asasi za usimamizi wa elimu hii katika kaunti,” akasema Bw Otunga.

Elimu ya nasari iligatuliwa pamoja na majukumu kama afya na kilimo kusimamiwa na serikali za kaunti badala ya serikali ya kitaifa.

Na licha ya magavana wengi kutangaza mikakati ya kuimarisha elimu hiyo kwa kuwaajiri walimu, wengi wamekuwa wakilalamikia changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizo ni a mazingira duni ya kufanyia kazi.

Vile vile, wamekuwa wakishinikiza kujumuishwa kwenye mfumo maalum wa kuwalipa mishahara, kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine wa serikali, jambo ambalo hazijafaulu hadi sasa.

Hadi sasa, hakuna mfumo ama utataribu maalum ambao umekuwa ukifuatwa na kaunti mbalimbali kuamua viwango vya mishahara ya walimu hao.