Habari Mseto

Walimu wakerwa na polisi kuzembea kazini kuchunguza mauaji

February 14th, 2019 2 min read

RICHARD MAOSI NA JOSEPH OPENDA

CHAMA cha Walimu nchini (KNUT) tawi la Nakuru, kimekerwa na jinsi polisi wamekuwa wakifanya uchunguzi wa kisa ambapo mwanafunzi alimuua mwalimu katika shule ya upili ya Hopewell.

Katibu mtendaji wa KNUT Paul Muiru alisema idara ya usalama imezembea kwa kujikokota kwa mwendo wa kobe kushughulikia maslahi yanayohusu usalama wa walimu.

Alieleza kuwa vyombo vya usalama havijakuwa vikitilia maanani swala hilo hasa ikizingatiwa walimu walitaka kuhakikishiwa usalama wao.

BW Muiru aliongezea kuwa wanachama wameshangazwa na jinsi polisi wameshindwa kuwafikisha washukiwa zaidi mahakamani na kuwashtaki.

“Tunashangaa mpaka sasa ni mshukiwa mmoja tu aliyefikishwa mahakamani kujibu mashtaka.Pia uchunguzi umesitishwa ghafla, kwani mwanafunzi aliyetekeleza kitendo hicho alishirikiana na raia pamoja na wanafunzi wa shule jirani ya Tumaini,” alisema.

Kisa hicho kilichotendeka Januari 24, kilisababisha kifo cha mwalimu Peter Omare Mogusu, alipojaribu kumpokonya mwanafunzi simu wakati wa masomo ya ziada.

Mwanafunzi wa kidato cha pili kutoka shule jirani ya Tumaini alikamatwa siku ya Jumatatu na kufikishwa mahakamani kuhusiana na kisa hicho.

Akisimama mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Nakuru Janet Mulwa,alipendekeza mwanafunzi huyo afanyiwe uchunguzi wa akili kabla ya kutoa uamuzi wake.

Viongozi wa muungano wanasema washukiwa zaidi wanahitajika kufika mahakani,kwani njama yenyewe ilihusisha wanafunzi wa shule ya Hopewell na wale wa shule jirani.

Aidha Muiru alinyoshea idara ya elimu katika kaunti kwa kutoonyesha juhudi zozote katika harakati za kupambana na kifo cha mwalimu Peter.

Alieleza kuwa mkurugenzi wa elimu hakutembelea shule ya Hopewell kisa kilipotendeka wala kuzuru familia ya marehemu kuwafariji.

“Walimu wana haki sawa na wanafunzi kuishi,lakini nina uhakika endapo ni mwanafunzi angetendewa ukatili sampuli hii watu wengi sana wangeingia gerezani kufikia sasa,” Muiru alisema.

Wanachama pia walisema viongozi wa kaunti wamekuwa wakiwakosea walimu heshima hadharani.

Manaibu kamishna wa kaunti pia wamekuwa wakiwatukana na kuwalaumu walimu kwa kila kitu kinachojiri.

“Kwa mfano katika shule moja eneo la Kaptembwa ambapo naibu kamishna mmoja alishambulia mwalimu baada ya mwanafunzi wake kupata alama tano katika mtihani wa KCSE,” alisema.

Juhudi za Taifa Leo Dijitali kumfikia mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Nakuru Dkt William Sugut hazikuzaa matunda kwani simu yake haikupokelewa.

OCPD wa Nakuru Samwel Obara alikataa kuzungumza na wanahabari akisema kesi ilikuwa kortini wala hangehitilafiana na uchunguzi.

“Sipo katika nafasi sahihi ya kutoa maoni wakati huu kwa sababu kesi iko mahakamani,” alisema.

Huenda serikali kuu ya kitaifa italazimika kuingilia kati ili kukabiliana na wahusika huku walimu wakiomba kuhakikishiwa usalama wao.