Habari Mseto

Walimu wakuu waagizwa kurejea kazini

July 18th, 2020 1 min read

Na FAITH NYAMAI

WIZARA ya Elimu imewaagiza walimu wakuu wa shule za msingi na upili kurudi kazini na kuanza kukusanya habari za wasichana wote ambao wamepata mimba katika kipindi hiki cha janga la corona.

Agizo hilo limewakanganya walimu kwa sababu hawajui watakavyolitekeleza kwa kuwa shule zimefungwa kama hatua moja ya serikali ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Kwenye agizo lililotolewa kupitia barua na Katibu wa Elimu, Dkt Belio Kipsang, walimu wakuu wa shule wanatakiwa kushirikiana kwa karibu na wizara za usalama na afya ili kupata habari zote kuhusu wasichana wa shule waliopata mimba na waliko.

Kulingana na agizo hilo, walimu hao wanatakiwa kuwasilisha ripoti kwa makao makuu ya Wizara ya Elimu kabla ya Julai 23, 2020.

“Dhamira ya barua hii ni kwa maeneo yote, kaunti na kaunti ndogo kukusanya habari kuhusu wasichana ambao kwa sasa wanatarajia kupata watoto na wale ambao walijifungua majuzi na ambao wanaweza kuacha shule zitakapofunguliwa,” ilisema barua iliyoandikwa Julai 14.

Barua hiyo ilitumwa kwa wakurugenzi wote wa elimu katika kila eneo, wakurugenzi wa elimu katika kaunti na kaunti zote nchini wiki moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza visa vyote vya mimba za wasichana wa shule vichunguzwe.

Idadi ya wasichana wanaopata mimba na kudhulumiwa kimapenzi imeongezeka nchini siku za hivi majuzi huku visa hivyo vikihusishwa na hatua za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Mnamo Julai 6, 2020, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza kituo cha kitaifa cha utafiti wa uhalifu (NCRC) kuchunguza visa hivyo katika muda wa siku 30 na kumkabidhi ripoti ya uchunguzi huo.