Lugha, Fasihi na Elimu

Walimu wakuu wakimbilia ‘TP’ kuokoa jahazi sekondari za JSS

May 22nd, 2024 3 min read

NA MAUREEN ONGALA

MASOMO katika shule za Sekondari ya Msingi (JSS) yametatizika kote nchini tangu walimu waanze mgomo wao.

Mnamo Jumatatu walimu wa JSS kutoka maeneobunge tisa katika Kaunti ya Kilifi waliandama mjini Kilifi wakitaka Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kutekeleza matakwa yao.

Hali ilikuwa sawa Pokot Magharibi ambapo Jumatatu walimu waliandamana mjini Kapenguria kutoa kero yao.

Mkwamo huu umefanya walimu wakuu katika kaunti ya Kilifi na maeneo mengine ya nchi kutafuta usaidizi wa wanafunzi wa vyuo vikuu kuziba pengo lilioachwa na walimu ambao wamegoma.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Kilifi na Sekondari ya Msingi mjini Kilifi Bw Emmanuel Karuke alisema kuwa wanafunzi wa chuo kikuu ambao wako katika mafunzo yao ya nyanjani almaarufu TP (kwa maana ya Teaching Practice) wamekuwa wa msaada mkubwa wakati huu.

Aliongeza kusema kuwa pia walimu walioajiriwa na bodi za shule wanatekeleza wajibu muhimu kipindi hiki kigumu.

“Masomo hayajatatizika sana kwa sababu tunao walimu ambao wanafunza watoto wetu kwa sasa,” akasema Bw Karuke.

Lakini hali ni ngumu katika shule ya Basi iliyoko katika eneobunge la Kilifi Kaskazini ambayo imeathirika sana kwani ina mwalimu mmoja tu aliyeajiriwa kwa mkataba wa kudumu (PNP) na Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC).

Mwalimu wa JSS kutoka kaunti ndogo ya Rabai alieleza kuwa shule hiyo ya Basi iko na mwalimu mmoja wa mkataba wa kudumu ambapo licha ya kuwa hawezi kuwafunza wanafunzi wote, ni changamoto kubwa kuwadhibiti kwani ni wengi.

“Hii ni changamoto kubwa sana inayohitaji suluhu ya haraka kwa sababu hata hao walimu wa mikataba ya kudumu bado hawana amani shuleni,” akasema mwalimu huyo.

Akizungumza na Taifa Leo naibu wa katibu mtendaji wa Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo (Kuppet) katika kaunti ya Kilifi Bw Zachary Opollo alisema kwa sasa walimu wametatizika huku wanafunzi wakiendelea kupata elimu duni.

“Hakuna masomo ya maana yanayoendelea kwa sekondari za JSS kwa sasa na walimu walimu wakuu wanalazimika kuwatafuta wanafunzi wa vyuo vikuu walio katika mwaka wao wa pili ambao wanastahili kupata mafunzo na kupeana ripoti zao ili kuwafunza watoto wetu,” akasema Bw Opollo.

Bw Opollo alisema kuwa inasikitisha kuwa baadhi ya shule ziko tu na walimu walioandikwa kwa mikataba ya elimu nyanjani bila kuwa na wale wa kudumu.

“Wanafunzi wetu wa JSS hawapati masomo ya kutosha na yake ya kiwango kinachostahili kwa sababu hali halisi ni kuwa hawasomi na hawajawahi kusoma ipasavyo. Tunapoteza kizazi chote cha gredi za Sita, Saba, Nane na Tisa kwa kuwapa watoto hao elimu duni,” akasema.

Kiongozi huyo wa walimu alitoa wito kwa serikali kusikia maombi ya idadi kubwa ya wadau katika sekta ya elimu ambao walitaka shule za JSS kuwekwa katika shule za upili nchini.

“Ni vyema ikiwa serikali itakubali makosa na kurekebisha kabla hatujachelewa na kusababisha madhara zaidi,” akasema.

Katibu mtendaji wa Kuppet kaunti ya Kilifi Bw Caleb Mogere alitoa wito kwa TSC kufanya kazi bila kushinikizwa kisiasa.

“Wanafunzi ambao wanaendeleza masomo yao ndio wanastahili kuajiriwa kwa mfumo wa masomo nyanjani yaani Internship lakini mtu yeyote ambaye amehitimu na ametambuliwa na TSC, anastahili kuwa mwalimu kwa mkataba wa kudumu,” akasema Bw Mogere.

Bw Mogere alieleza masikitiko yake kuwa serikali imeamua kumnyima mtoto wa maskini haki ya kupata masomo bora huku ikiwanyima walimu kazi.

“Watoto wa maskini hawasomi kwa sababu walaimu hawapo shuleni. TSC haiwezi tuambia kuwa imeajiri walimu 56,000 ambao ni wa muda na wanalipwa Sh17,000,” akasema.

Alifoka na kusema kuwa ataendelea kupigania haki ya walimu hao.

“Tumekataa walimu wa JSS kudhulumiwa kwa sasa… walimu wamechoka na kupitia hali ngumu huku wakifunza masomo ambayo hawajasomea. Unapata mwalimu wa Fisikia anafunza Kiswahili,” akasema.

Bw Andrew Lelei alisema ni lazima serikali itekeleze matakwa yao ili kkuepusha wanafunzi kupata elimu duni.

Alisema walimu wengi wamelazimika kufunza masomo ambayo hawana ufahamu nazo.

“Inashangaza kuwa tunafunza tu masomo yoyote. Kwa mfano mimi ni mwalimu wa Hisabati na ninafunza Fizikia. Hata moto ukitokea ndani ya maabara nitatoroka pamoja na wanafunzi,” akasema Bw Lelei.

[email protected]