Habari Mseto

Walimu wakuu waonywa vikali dhidi ya kuongeza karo Januari

December 19th, 2019 1 min read

Na Kalume Kazungu

WALIMU wakuu wa shule za sekondari Ukanda wa Pwani wameonywa vikali dhidi ya kuongeza kiwango cha karo msimu huu ambapo matayarisho ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kujiunga na shule hizo za upili kufikia Januari mwakani yanaendelea.

Mshirikishi wa Elimu Ukanda wa Pwani, Bw Hassan Duale, alisema tayari ametuma wakurugenzi wa elimu kwa kila kaunti eneo hilo kuchunguza walimu ambao wameongeza kiwango cha karo kichinichini ili waadhibiwe.

Bw Duale alisema ofisi yake haitakubali baadhi ya shule, hasa zile za umma kukiuka kiwango cha karo kilichotolewa na serikali.

Bw Duale alisema tabia ya walimu wakuu ya kuongeza karo kiholela inawazidishia wazazi mzigo na hata kuwa kikwazo katika kuafikiwa kwa mpango wa serikali wa asilimia 100 ya wanafunzi wanaovuka kutoka shule za msingi hadi sekondari nchini.