Habari Mseto

Walimu waliosimamia mtihani wa KNEC wadai malipo

April 28th, 2019 1 min read

KEVIN ROTICH NA RICHARD MAOSI

ZAIDI ya walimu 100 wa shule za msingi kutoka Kaunti ya Nakuru waliosimamia mitihani katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Rift Valley (RVIST) wanadai malipo yao.

Walimu hao walikuwa wameratibiwa kusimamia mtihani wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) unaofanyika kila muhula.

Wanalaumu muungano wa walimu KNUT na kamati ya kutahini KNEC kwa kuwapuuza walipohitaji malipo yao.

Bw Macharia mwalimu wa shule ya msingi ya Subuku aliyesimamia zoezi hilo anasema bado hakuwa amepata malipo,licha ya kupokea ahadi nyingi kutoka kwa KNUT kuwa pesa zake zingelipwa.

“Nimetuma malalamishi kwa maafisa wa KNEC na KNUT mjini Nakuru,lakini juhudi hazijaonekana kuzaa matunda yoyote,”alisema.

Macharia anasema kila anapozuru afisi za KNUT mjini Nakuru,yeye huelekezwa katika kaunti ndogo ya Rongai.

Lango la Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Rift Valley (RVIST), Nakuru. Picha/ Richard Maosi

“Hata nimejaribu kuzungumza na afisi ya mitihani katika kaunti ndogo ya Rongai,lakini simu zangu huwa hazipokelewi,” alisema.

Aidha aliongezea kuwa mwalimu anapokataa kusimamia mitihani ya KNEC huwa analaumiwa vikali ijapokuwa si hiari yake.

“Mitihani mingine inakaribia lakini mpaka sasa hatujapokea malipo ya awali,tunashangaa endapo tutalipwa,” alisema.

Mwalimu mwingine Monica Subuku anasema amechoka kusimamia mitihani,ambayo mwishowe haina malipo. Pia anasema haoni haja ya kuendelea kusimamia mitihani ya KNEC.

“Tumekuwa tukilazimishwa kusimamia mitihani,lakini matatizo hutokea wakati wa kudai malipo ya jasho letu,”alisema.

Monica anasema wamekuwa wakijigharamia kufika katika vituo vya kusimamia mitihani,lakini anajuta kwa kupoteza muda wake.

Taifa Leo walizungumza na katibu mtendaji wa KNUT tawi la Nakuru Bw Muingai Muhia,ambaye alikubali kuwa wasimamizi wa KNEC hawakuwa wamepokea malipo yao na aliwahakikishia kuwa wameweka mikakati kushughulikia hilo.

“Kumekuwa na tatizo kidogo katika mtindo wa kuwasilisha malipo,lakini KNEC imehakikisha kuwa walimu wote watapokea malipo yao kwa wakati,”alisema.

Wakizungumza na Taifa Leo walisema wameimarisha juhudi kuhakikisha walimu wote wanapokea malipo yao.