Habari Mseto

Walimu, wanafunzi watoa kauli tofauti kuhusu KCPE

July 10th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

WANAFUNZI na walimu wanaofunza da Darasa la Nane na Kidato cha Nne waliostahili kufanya mtihani wa kitaifa mwaka huu wameeleza hisia mseto baada ya serikali kufutilia mbali mitihani hiyo hadi mwaka ujao.

Huku baadhi wakisema hatua hiyo itawarudisha nyuma kimasomo, wengine walisema watapata nafasi kujiandaa vyema kwa mtihani.

‘Nilikuwa nikijindaa nikitarajia kuwa nitafanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane mwishoni mwa mwaka huu, lakini sasa nahisi kama nilipoteza wakati,’ akasema Swabrina Omar mtahiniwa wa darasa la nane katika shule ya msingi ya Bomu, eneo bunge la Changamwe, Kaunti ya Mombasa.

Tangu shule zifungwe Machi kwa sababu ya janga la Corona, wadau katika sekta ya elimu wamekuwa wakijadiliana kuhusu kufunguliwa kwa shule hizo kwa ajili ya mitihani ya kitaifa.

Uamuzi ulitangazwa Jumanne na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha kuwa mitihani ya kitaifa haitafanywa mwaka huu kwa kuwa maambukizi ya virusi vya corona yanaongezeka.Mwanafunzi mwingine, Fatuma Mohammed kutoka Shule ya Upili ya Mama Ngina, Mombasa, alisema anahofia hatua ya kusukuma mbele mtihani hadi mwaka ujao huenda ikafanya wengine wao kulegea kimasomo.

‘Kuna uwezekano mkubwa kwetu kutofanya vizuri kufuatia hatua hii,’ akasema. Hata hivyo, mwanafunzi mwingine, Bilal Ali alisema angalau sasa wanafunzi watapata muda wa kutosha kujitayarisha.

‘Kuna watahiniwa ambao hawana uwezo wa kufuatilia masomo mtandaoni. Tumekuwa nje ya shule tangu Machi,’ akasema.

Mwalimu anayesimamia wanafunzi wa darasa la sita hadi nane katika Shule ya Msingi ya M.M Shah na M.V Shah, Bw Bonface Ekirapa alisema muda walioongezewa utawasaidia kuwaandaa wanafunzi wao vilivyo.

Mwalimu mkuu katika shule ya Kisauni Bw Joshua Kuria alisema watatumia muda ulioongezwa kuwaandaa wanafunzi wao.

Wanafunzi wengine waliohojiwa katika kaunti tofauti pia walikuwa na hisia mseto.

Katika Kaunti ya Siaya, Mary Akoth alisema: ‘Serikali ingelegeza masharti ili watahiniwa wafanye mitihani yao. Hilo lingetupatia matumaini.’