Habari za Kitaifa

Walimu wanagenzi wa JSS na madaktari kuajiriwa licha ya Mswada wa Fedha 2024 kufutiliwa mbali


NI afueni kwa walimu vibarua wa Shule za Sekondari Msingi (JSS) na madaktari wanafunzi kwani sasa watapewa ajira ya kudumu licha ya kuangushwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024.

Hii ni baada ya serikali kudumisha mgao wa Sh18.9 bilioni za kuajiri walimu wa JSS na Sh3.7 bilioni za kuwapa ajira ya kudumu madaktari vibarua.

Pesa hizo zitalindwa katika Bajeti ya kwanza ya ziada itakayowasilishwa bungeni baada ya wabunge kurejelea vikao vya kawaida mnamo Julai 23, 2024.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano uliofanyika Ijumaa wiki iliyopita, kati ya maafisa wa Hazina ya Kitaifa wakiongozwa na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti.

Duru za kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro zimeambia Taifa Dijitali kwamba iliafikiwa mgao wa fedha za kuajiri walimu na madaktari hao hautapunguzwa.

“Serikali itaendelea na mipango yake ya kuajiri walimu 46,000 wa JSS na madaktari wanafunzi katika mwaka huu wa kifedha wa 2024/2025. Mpango huo utafadhiliwa na fedha zitakazopunguzwa kutoka mgao wa wizara, idara na mashirika mengine ya serikali katika bajeti ya ziada,” mbunge mmoja ambaye ni mwanachama wa kamati ya bajeti akaambia Taifa Dijitali, lakini akaomba tubane jina lake kwani sio msemaji rasmi wa kamati hiyo.

Wiki jana Profesa Ndung’u alitangaza kuwa mgao wa bajeti kwa Wizara, Idara na Mashirika (MDA) utapunguzwa kufuatia kukataliwa kwa Mswada wa Fedha 2024.

Serikali ilitarajia kukusanya Sh347 bilioni kutokana na mswada huo, kuongezea Sh2.95 trilioni kutoka kwa mapato ya kawaida na misaada ya kigeni, kufadhili bajeti yake ya kima cha Sh3.9 trilioni.

Lakini mnamo Juni 26, 2024 Rais Ruto alitangaza kuwa hatatia saini mswada huo, licha ya kupitishwa na wabunge, baada ya vijana kufanya msururu wa maandamano nchini kuupinga.

Vile vile, maafisa wa Hazina ya Kitaifa na wanachama wa kamati ya bunge kuhusu bajeti walikubaliana kwamba Sh1.8 bilioni zilizotengewa mpango wa lishe shuleni hazitaondolewa wala kupunguzwa.

Hata hivyo, wabunge wanaowakilisha maeneobunge 290 watapoteza Sh15 bilioni zilizoongezwa kwa Hazina ya Ustawi wa MaeneoBunge (NG-CDF) katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha.

Pesa hizo ziliratibiwa kufadhili mpango wa kuunganisha umeme katika maeneobunge hayo, ambapo kila eneobunge lilitarajiwa kupokea Sh50 milioni.

Aidha, Sh1.6 bilioni zilizotengewa ukarabati wa miundomsingi katika shule za umma ziliondolewa.

Kumekuwa na wasiwasi kuhusu hatima ya walimu wa JSS na madaktari wanafunzi baada ya Rais William Ruto kutangaza mipango ya kupunguzwa kwa fedha zilizotengewa mipango na miradi mbalimbali kufuatia kukataliwa kwa Mswada tata wa Fedha wa 2024.