Makala

Walimu wanaotegemea lifti za ndege za KDF wakosa kufika shuleni

June 3rd, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

UKAGUZI unaoendelea wa ndege za kijeshi kwenye idara ya ulinzi nchini umechangia watoto wa Msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu kusalia nyumbani tangu shule zilipofunguliwa kwa muhula wa pili wiki tatu zilizopita.

Walimu wa shule za vijiji vya msitu wa Boni hutegemea helikopta za idara ya jeshi (KDF), kuwasafirisha kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Mokowe hadi kwenye shule zao za msitu wa Boni.

Hili ni kwa vile usafiri wa barabara eneo hilo ni hatari kwani magaidi wamekuwa wakitega vilipuzi barabarani.

Ukaguzi wa ndege za KDF ulitokana na kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Francis Ogolla mbali na ajali nyingine za ndege za kijeshi nchini.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa kati ya shule tano zilizoko msitu wa Boni, ni shule moja pekee ambayo imefunguliwa na wanafunzi kuendelea na masomo.

Shule hiyo ni ile ya Kiangwe ambayo inapakana na Bahari Hindi. Walimu walifaulu kusafirishwa na kufikishwa shuleni humo kupitia mashua baharini.

Shule ya Msingi ya Mararani msituni Boni, Lamu Mashariki. Ni miongoni mwa shule nne zilizosalia kufungwa baada ya walimu kukosa kuripoti  sababu za changamoto ya usafiri na usalama. Picha|Kalume Kazungu

Aidha shule ambazo kwa sasa bado hazijafunguliwa ni Mangai, Milimani, Mararani na Basuba.

Jumla ya wanafunzi 350 wa shule hizo ambao ni kutoka chekechea (ECDE) hadi Gredi 6 wamesalia nyumani na wazazi wao kwani shuleni hakuna walimu wa kuwafundisha.

Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Lamu, Bw Zachary Mutuiri alithibitisha kuwa walimu wanaohudumia shule nne za msitu wa Boni bado hawajafikishwa shuleni, hatua ambayo imezuia masomo kuendelea shuleni.

“Hata wanafunzi wakafika shuleni, walimu bado hawajafika kwani changamoto iliyopo ni usafiri. Tunajadiliana na Wizara ya Usalama wa Ndani kupitia ofisi ya Kamishna wa Lamu ili kuona jinsi tutawapeleka walimu,” akasema Bw Mutuiri.

Naibu Kamishna wa Lamu Mashariki, Bw George Kubai, alisema mikakati kabambe inaendelea kuwasafirisha walimu msituni Boni haraka iwezekanavyo.

“Tulitaka kujaribu barabara lakini mafuriko nayo yaliharibu. Isitoshe, usalama wa barabarani bado ni wa ati ati,” akasema Bw Kubai.

Viongozi na wazazi waliiomba serikali kufikiria kuwasajili vijana wa msitu wa Boni na kuwafadhili kusomea kozi ya ualimu ili warudi vijijini mwao kuisaidia jamii punde wanapohitimu.